January 04, 2011

Ikulu: JK hamiliki Dowans

Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete hana uhusiano wowote na kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limited.

Katika taarifa yake iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilisema Rais Kikwete sio mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo.

Taarifa ya Ikulu ilitolewa kufafanua habari iliyoandikwa Jumapili wiki iliyopita na gazeti moja (siyo NIPASHE), likimkariri Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, akidai kuwa Rais Kikwete ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo.

“Huu ni uongo wa mchana. Ni uzushi wa karne na propaganda ya hatari. Kwa hakika na kwa namna isiyoweza kuelezeka kwa ufasaha, tumeshtushwa sana na kauli hii ya Dk. Slaa na hatutaki kuamini kabisa wala kukubali kuwa ni kweli kauli hii imetolewa na mtu, ambaye majuzi tu alikuwa akiwania kuwa kiongozi wa juu wa taifa letu, yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza: “Mheshimiwa Rais Kikwete siyo mmiliki wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Dowans. Hakupata kuwa mmiliki, siyo mmiliki na wala hatakuwa, hata siku moja, mmiliki wa Kampuni hii.”

Ikulu ilisema kama Dk. Slaa anataka kweli kujua wamiliki wa Kampuni ya Dowans, basi atafute ukweli huo na aachae tabia ya kutapatapa na udhabinadhabina yenye lengo la kuwapaka watu matope na kwamba, tabia ya kuwasingizia na kusema uongo kuhusu viongozi wa kitaifa ni ya hatari.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete hahusiki na Kampuni ya Dowans wala na kampuni nyingine yoyote ya kibiashara.

“Yeye ni kiongozi wa juu kabisa wa siasa wa nchi yetu na siyo heshima wala haki kumhusisha na jambo la kutunga na kuzua na lisilokuwa la ukweli wowote,” iliongeza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Salva Rweyemamu.

Taarifa hiyo iliwataka na kuwaomba Watanzania, kupuuza uzushi na uongo wa sasa kuhusu miliki ya Dowans.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22