Kilichotokea ni kwamba, mwaka huu mwanzoni kabisa, A.Y aliwasiliana na mimi akiwa na mipango ya kuzindua albamu yake. Na alitaka kuzinunua zile nyimbo kutoka kwangu akiwa na mpango mpya wa kuiuza albamu kwa mpango wake binafsi basi na mimi. Nilishindwa kuelewa nini anakifanya hasa alipoomba alipie wimbo mmoja mmoja tena kwa bei ya msanii wa kawaida anaehangaika kutoka.Niliamua kukubali kwamba ameamua kufanya hivyo na sina nguvu ya kumzuia basi nikajaribu kupata malipo halisi ya kazi yangu. Ubishi wangu ulikua kwamba msanii mdogo hawezi kulipa bei sawa ya kurekodi na msanii mkubwa, kwani hata malipo ya msanii mkubwa na mdogo baada ya kazi yoyote iwe ya matangazo ama show huwa hayafanani. Bei niliyotaja haikua millioni kumi, ni uongo mtupu na kwa wimbo mmoja niliomba nilipwe millioni 2.Akakubali kwa bei hiyo ya Millioni 2 japo nilihisi hakuridhika kabisa. Nilimtumia mkataba wa makubaliano yetu ambayo kweli baadae aliona kwamba bei hiyo kwake ni kubwa sana hivyo hatukusaini makubaliano. Tulibadilishana meseji kwa simu kwa muda mrefu sana na niliona biashara hii itavunja urafiki wetu.Nilifikiria sana kwamba nyimbo hizi nimekaa nazo toka 2008 bila kuingiza chochote na maisha yanaenda pia. Sikuona sababu ya kuharibu urafiki wetu wa muda mrefu kwa mabishano haya. Kwa Ujumbe wa simu nilimueleza A.Y anakaribishwa aje achukue nyimbo zoooooote anazohitaji kwa albamu yake BURE (bila malipo).Lakini nilimuomba anisamehe sitomix zile ambazo bado hazijamixiwa, ila ampatie producer mwingine amfanyie hiyo kazi.Mpaka naona hii makala A.Y hajaja kuchukua hizo nyimbo na ndio naelewa kua hayupo na BHits tena na wala taarifa zote hizo mbili hajawahi kunipatia. Huu ndio ukweli halisi.Swala la mimi kuwa na wivu na kinyongo na mafanikio ya A.Y ni uongo na nashangaa umetoa wapi maneno hayo. Kama kulipwa kidogo, huku nikiona A.Y anaingiza fedha nyingi kwa muziki tunaotengeneza pamoja basi ningekua nimegombana nae toka mwaka 2009 labda.Narudia kwamba nilikua najua kila show yake inapofanywa na sikuwahi kujisikia vibaya. Nataka utambue pia nilikua na akili timamu wakati nafanya kazi na A.Y na muda wowote nilikua na uwezo wa kubadili mawazo na kutaka tuandike makubaliano kwa karatasi ila sikufanya hivyo na wala sijutii chochote kwa utaratibu wetu wa hatari wa kufanya kazi bila mkataba wa maandishi na ndio maana nipo radhi hata sasa kumpatia nyimbo hizo bure kama nlivomwambia hapo mwanzo.
Nina meseji zote na email za mazungumzo yetu ambazo nilihifadhi nikijua ipo siku nitaonekana mimi ndie mkorofi, hivyo nachokisema nina hakika nacho asilimia 100.Picha nyingine mbaya ulioichora ni kujaribu kuonyesha kuna kutopendana kati ya maproducer. Mimi Master Jay na Marco Chali ni marafiki wazuri tu na mpaka leo hii nikiwa na shida na nikamhitaji Marco Chali au Master Jay nitampigia simu bila aibu kwani hakuna ugomvi kati yetu. A.Y, Master Jay na Marco Chali pia ni marafiki wa siku nyingi na katika kipindi cha miaka minne akiwa Bhits kwa hiari yake na sio mkataba, A.Y amekuwa akienda MJ records anapojiskia na mara kadhaa mimi nimeenda na A.Y na mara kadhaa nimeenda peke yangu tena kwa ajili ya shughuli zangu binafsi.Pia ufahamu katika kipindi hicho A.Y alikua akitumia muda mwingi MJ Records kuliko Bhits na hiyo yote ilikua ni mipango yake binafsi. A.Y hajawahi kuzuiwa kufanya kazi na mtu mwingine kwani ni msanii huru.Ndugu yangu mimi ni mtu mpole nisiye na ugomvi na mtu hapa mjini. Nasikitika sana kwa jinsi kwenye makala yako ulivyojitahidi kuonyesha kwamba mimi na swahiba wangu tumejenga uadui.
No comments:
Post a Comment