Baba mzazi wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Umoja wa Vijana (UVCCM), marehemu Amina Chifupa, jana alikuja juu akisema kwamba majina ya vigogo waliosababisha kifo cha mwanae wataanikwa hadharani tena mbele ya waandishi wa habari hivi karibuni.
Mzee Hamis Chifupa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba kabla ya mwanae hajafa kuna aliowataja kwa mabaya na mazuri wakiwamo vigogo na wafanyabiashara wazito na kwamba wote watachunguzwa kubaini ni kina nani walihusika.
"Wakati anaumwa alitaja majina ya watu wengi, ili kubaini kama walihusika familia inafanya uchunguzi na baadaye tutatoa majina ya waliohusika hapa hapa," alisema Mzee Chifupa.
Akadai kwamba kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba mwanae Amina alikufa kabla ya wakati wake kwa vile kuna watu alikuwa akiwataja taja wakati alipokuwa anaumwa.
Hata hivyo alisema uchunguzi kuhusu kifo cha marehemu Amina haufanyiki kama ule wa Tume ambapo watu huitwa na kuhojiwa bali unafanyika kwa kufanyia kazi taarifa za mtoto wao alizosema wakati wa uhai wake. Alipoulizwa wanafamilia ilitaka Amina afariki lini ili iweze kuamini amekufa wakati muafaka alijibu;
"Kufa angekufa lakini sio kwa kipindi hiki kwani wamemuwahisha muda wake ulikuwa bado" Waandishi wa habari walipomuuliza mzee Chifupa kuwa ripoti ya madaktari inaeleza marehemu Amina alikufa kwa ugonjwa gani, alijibu ya kuwa inaonesha kwamba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na yale ya kiswahili.
Mzee Chifupa alisema mwanae alikuwa mtu wa maajabu na kutolea mfano kimbunga kilichotokea ghafla mara baada ya kuingia ukumbini kwa ajili ya sherehe yake ya kicheni pati.
Waandishi wa habari walipombana mzee huyo kuwa kama anaamini mtoto wake alikuwa mtu wa ajabu ni kwa nini hataki kuamini taarifa zilizoelezwa katika kanisa moja jijini Dar es Salaam kuwa Amina hajafariki bali alichukuliwa msukule na yupo mashamba ya Kibaha alijibu ya kuwa hilo hakubaliani nalo. Hata hivyo alisema milango ipo wazi kwa watu wanaodai wana uwezo wa kumrejesha.
Alisema wakati kifo chake kilipotokea alipokea simu zaidi ya 10 kutoka kwa waganga waliodai wana uwezo wa kumrejesha na aliwataka wafanye hivyo kama wanaweza lakini wameshindwa. Mzee Chifupa alisema familia yake inaamini Amina alifariki na yupo peponi.
Kuhusu urithi wake alisema mahakama ilishatoa uamuzi na ilieleza kuwa watu wanaotakiwa kurithi mali zake ni mama yake, baba na mtoto wake.
Hata hivyo hakueleza mali zake alizoacha zina thamani kiasi gani. Kifo cha Amina Chifupa kilichotokea Juni mwaka jana kilifunikwa na utata mwingi kwa sababu kabla ya kifo chake habari zilisema mume wake alikwenda kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana, John Nchimbi akamweleza jambo ambalo lilimuudhi na kuamua kumpa talaka marehemu.
Amina Chifupa alikuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya watumia madawa ya kulevya na wakati fulani aliwahi kutamka kwamba ana majina yao na alikuwa tayari kutaja majina yao.
2 comments:
Kile ambacho mimi nakiona hapa ni baba wa marehemu Amina anapenda publicity, sasa wakati mtoto wake yuko hai hakuna aliyekuwa anamjua sasa anatumia jina la marehemu kujitangaza yeye lakini ni ujinga kwani hata muda wake umekweisha kabisa! atulie asali sana kupunguza dhambi!
mtu mzima hovyo, mzee chifupa anawazimu aondoe hupuzi wake haibu tupu haoni hata haya
tina
Post a Comment