July 22, 2008

Ukweli wa mauaji ya albino wafichuliwa

Mauaji ya maalbino nchini Tanzania yanaendelea licha ya kuanzishwa kwa kampeni za kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaotumia viungo vya binadamu kwa imani za kishirikina.
Hadi sasa zaidi ya maalbino 20 wameuawa tangu mwishoni mwa mwaka jana, licha ya amri ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kuwalinda maalbino hao.
BBC imetoa ushahidi unaothibitisha vitendo hivyo vya ukatili vinavyochochewa na waganga wa kienyeji wanaowarubuni wateja wao.
Waganga hao huwaahidi wateja wao kuwatajirisha kwa haraka kwa kutumia dawa zilizochanganywa na nywele, damu na mifupa ya albino.
Chama cha maalbino kimesema zaidi ya watu 170 wamekamatwa kuanzia mwezi Machi mwaka huu lakini hakuna hata mmoja aliyehukumiwa.
Jumuiya ya maalbino imeomba kulindwa na jeshi la polisi la nchi hiyo.
Takwimu za polisi zinaonyesha kwamba mkoa wa Mwanza unaongoza kwa mauaji haya ya maalbino na pia vikongwe, hasa wale wenye macho mekundu.
Kati ya maalbino 24 waliouawa tangu mwaka jana mwishoni, 11 wanatokea katika mkoa huu uliopo kando mwa Ziwa Victoria.
Lakini pia ni mkoa unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waganga wa kienyeji huku wale waliosajiliwa ni takriban 3,000.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22