Jiji la Cologne linajiandaa kukabiliana na "mkutano mkuu wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia dhidi ya dini ya kiislam" unaoanza leo,wakihudhuria viongozi wa vyama hivyo kutoka nchi kadhaa za Ulaya.Maelfu ya waandamanaji wanapanga kuteremka majiani kulaani mkutano huo unaoitishwa na chama kinachopalilia chuki dhidi ya wageni "Pro Köln. Askari polisi elfu tatu wamewekwa tayari kukabiliana na kitisho cha kuzuka machafuko,huku meya wa jiji la Cologne,Fritz Schramma wa kutoka chama cha Christian Democratic CDU, aliyewatolea mwito wananchi "wasiwavumilie hata kidogo wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia",akiashiria maandamano ya watu elfu 60 kupinga kongamano la vichwa upara litakalofanyika jumamosi asubuhi. Ubalozi wa Marekani umewashauri raia wa nchi hiyo wasiutembelee mji wa Cologne wakati huo.Kundi la siasa kali za mrengo wa kulia-Pro-Köln,linalokosoa kile wanachokiita "kugeuzwa Ujerumani kuwa ya kiislam" na hasa ujenzi wa msikiti mkubwa katika jiji la Cologne,limewaalika viongozi mashuhuri wa siasa kali za mrengo wa kulia kutoka nchi mbali mbali za ulaya kuhudhuria mkutano huo mkuu unaoanza hii leo. Kilele cha mkusanyiko huo kitafikiwa jumamosi jioni katika mji mkongwe ambapo hotuba kali kali zinatazamiwa kutolewa kuhusu namna ya kuhifadhi maadili ya dini ya kikristo. Polisi inaamini vichwa upara hao hawatapindukia mamia.Lakini maandamano zaidi ya 20 kupinga hisia za chuki dhidi ya wageni yatafanyika hasa jumamosi asubuhi kutokana na mwito wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi wa ujerumani DGB na viongozi wa makanisa. Meya wa jiji la Cologne Fritz Schramma aliyetetea kwa ufanisi umuhimu wa kujengwa msikiti mkuu,amewatolea mwito wakazi wa eneo la mji mkongwe wafunge maduka na madirisha ya nyumba zao kudhihirisha upinzani wao dhidi ya vichwa upara.
Meya Fritz Schramma anasema:Tutawatenga na tutasimama kidete dhidi yao.Mji mzima unachangia naiwe kutoka vyama vya wafanyakazi,mashirika ya spoti,makanisa,vyama vya kisiasa,kila upande umeamua kuchangia na kuteremka mjini jumamosi ijayo-kwa maandamano ya amani lakini yatakayodhihirisha kinaga ubaga,kupitia hotuba na muziki,na watu kukamatana mikono mfano wa mnyororo,hayo hatuyataki katika mji wetu."Leo hii chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Pro Köln kimepanga kuanzisha kampeni yake kwa kuwatembeza kwa mabasi wageni wake katika ile mitaa wanakoishi wageni wengi.Wakijibu uchokozi wa Pro-Köln,wamiliki 150 wa baa katika jiji la Cologne wamebandika beramu zenye maandishi "Hatuwauzii manazi Kolsch" wakimaanisha kinywaji cha bia inayotengenezwa katika jiji la Cologne.Bilauri laki mbili zimeandikwa hivyo hivyo.Polisi elfu tatu kutoka kila pembe ya Ujerumani wamewekwa katika hali ya tahadhari pakihofiwa manazi mambo leo,na vichwa upara wasije wakachochea machafuko dhidi ya waandamanaji wa makundi ya mrengo wa shoto.
No comments:
Post a Comment