February 15, 2009

Uwanja mpya kuzinduliwa leo

Uwanja wa Taifa wa zamani umebadilishwa jina na kupewa jina jipya la uwanja wa Uhuru, ambapo jina lililozoeleka la uwanja wa Taifa limetangazwa kutumiwa na uwanja mpya na wa kisasa unaotarajia kukabidhiwa leo kwa serikali. 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka serikalini imeelezwa kuwa maamuzi ya kuubadili jina uwanja wa zamani yametokana na umuhimu wa uwanja huo, ambapo umetumika kwa matukio mengi ya nchi na pia ujenzi wake ulifanywa mwaka 1961, kwa ajili ya sherehe za uhuru wa Tanganyika. 

Imeelezwa kuwa makabidhiano ya hati za uhuru kati ya wakolini wa uingereza na muasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yalifanyika kwenye uwanja huo Desemba 9,1961. 

Aidha umuhimu wa kuupa jina hilo kuwa uwanja wa Uhuru, umetokana na uwanja huo kutumika kwa sherehe mbalimbali za maadhimisho ya uhuru wa Tanganyika, sherehe za Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar na sherehe nyingine. 

Pia imeelezwa kusa sababu nyingine ya kuupa uwanja huo jina la Uhuru ni kutokana na kufanyika kwa tukio la kuwapa wananchi fursa ya kuuaga mwili wa muasisi wa taifa letu na mpigania uhuru, Mwalimu Nyerere. 

Serikali, imeeleza kuwa nia yake ni kutunza historia ya taifa hili kwa kuupa jina la Uhuru uwanja huo mkongwe,ambapo jina la uwanja wa taifa litatumika kwenye uwanja mpya. 

Kwa upande wa sherehe za makabidhiano ya uwanja wa Taifa, serikali imesema kuwa sherehe za makabidhiano hayo zitafanyika kwenye uwanja huo, ambapo rais wa China Hu Jintao, atashiriki kikamilifu shughuli hiyo sanjari na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete. 

Sherehe za makabidhiano hayo zitavishirikisha vyama mbalimbali vya michezo, ambapo kutakuwa na maandamano pamoja na burudani mbalimbali kutoka kwa vikundi vya sanaa hapa nchini na vile vya China. 

Aidha, imeelezwa kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha ili kuhakikisha usalama unakuwepo katika wakati wote wa shughuli hiyo ya kihistoria. 

Uwanja huo ulianza kujengwa Januari 2005 na kampuni ya ujenzi ya Beijing Construction kwa kushirikiana na wataalamu wa ujenzi wa hapa nchini. 

Ujenzi wa uwanja huo wa kisasa ni sehemu ya ahadi zilizotolewa na rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa kwa watanzania na wanamichezo kwa ujumla. 

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na serikali imeelezwa kuwa uwanja huo umegharimu zaidi ya Sh. bilioni 50, ambapo zimetolewa kwa ushirikiano wa serikali hizo mbili. 

Mbali ya kugharimu kiasi hicho cha fedha uwanja huo unauwezo wa kuingiza watazamaji 60,000 waliokaa, ambapo pia unaluninga kubwa ya kisasa inayoweza kuonyesha shughuli zote zinazoendelea kwenye uwanja huo.

No comments: