February 03, 2009

Yu wapi anayesema Tanzania ni maskini?

KWA takriban miezi miwili sasa tumeshuhudia mabilioni ya shilingi na mali zikitolewa kama dhamana wa watuhumiwa wa ufisadi katika kesi mbalimbali, zinazowakabili katika mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam. Walianza watuhumiwa wa EPA, wakaja kina Mramba ambao nao waliweka dhamana ya mali zisizopungua sh bilioni moja na mwisho ni vigogo wa BoT kina Liyumba ambao wote kwa pamoja wameweka dhamana ya mali isiyopungua sh bilioni 110. Tukitamaza kwa undani mali za watu hao ambao wengine walikuwa watumishi wa serikali tunaweza kupata picha halisi ya nchi masikini ya Tanzania tunayoizungumzia kila siku na kutembeza bakuli kwa wahisani tukiomba tupatiwe misaada. Kama waziri mmoja anaweza kumiliki nyumba mbili za zaidi ya sh bilioni moja, anamiliki akaunti yenye zaidi ya bilioni moja nje, watendaji wengine nao wanawazidi mawaziri kwa kuwa na mali zenye thamani zaidi, huo umasikini tunaozungumzia uantoka wapi? Tatizo tulilo nalo si umasikini bali ni uongo wa viongozi wa kutudanganya Watanzania kuwa nchi hii ni masikini, ili tuendelee kuwa na mawazo mgando na tukose ujasiri wa kuchunguza rasilimali tulizonazo zinatunusaisha vipi. Viongozi wamekuwa wakitumia maneno matamu kuwa keki ya taifa ni ndogo au suungura mwenyewe ni mdogo hivyo si rahisi kwa wananchi wote kunufaika na rasilimali zilizopo. Kwa uongo huo wamefanikiwa, kwani asilimia kubwa ya Watanzania tunaamini nchi hii ni masikini, jambo linalowapa nafasi ya kuendelea kufanya ufisadi uliopindukia usio na chembe ya huruma wala aibu. Sh bilioni 221 ni fedha nyingi sana kama zingetumika kujenga barabara, zahanati, hospitali, shule na huduma nyingine, lakini kwa bahati mbaya fedha hizo zimeingia katika mikono ya watendaji na viongozi wasio waaminifu ambao masilahi binafsi ndiyo kipaumbele chao cha kwanza. Waziri anapoweka bilioni moja nje ya nchi, kumiliki shamba lenye ekari 40, magari zaidi ya sita, anasomesha watoto zake nje ya nchi, safari za mara kwa mara, tujiulize mali hizo kazipataje? Anamiliki shamba ekari 40, kuwa na hisa zaidi ya asilimia 20 katika miradi na kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi hapa nchini. Haya maswali yakijibiwa nina uhakika tutakuwa na mwelekeo mzuru kuhusu nchi yetu kuwa masikini au tajiri. Tanzania ni nchi tajiri lakini utajiri huo umehodhiwa na watu wachache ambao wamepata elimu na madaraka kwa jasho la walalahoi na sasa wameamua kuwanyonga waliowapa madaraka na kuwagharamia elimu yao kwa kuwaibia fedha na rasilimali kwa tamaa za kujilimbikizia mali. Ni aibu kwa nchi kuwa na watu wenye uhakika na milo na mambo ya starehe kwa zaidi ya miaka 100 ijayo, wakati kuna wananchi ambao hawana uhakika na mlo mmoja kwa siku na sehemu ya kuishi. Uongo wa viongozi sasa unaanza kugundulika kwa kuwa mambo yote waliyoyafanya nyuma ya pazia sasa yanaanza kuwa hadharani ingawa mengine bado yanafichwa fichwa. Sitanyamaza kukemea viongozi wanaoamini uongo ndiyo utakaowasaidia kuongoza nchi kwani nina imani ipo siku wananchi wataanza kuwapiga viongozi hao maana tayari kuna baadhi ya wananchi wameshaanza kuwaita viongozi waliomaliza muda wao kuwa ni mafisadi. Nina hakika miaka inayokuja serikali itakuwa na wakati mgumu sana wa kuongoza kwa kuwa wananchi watakuwa wamechoshwa na umasikini unaozidi kushamiri siku hadi siku. Tanzanite, mbuga za wanyama, almasi, dhahabu, misitu ni miongoni mwa rasilimali ambazo zimeshindwa kutumiwa vizuri na Wtanzania na hivi sasa zimekabidhiwa mikononi kwa wageni kwa kigezo cha uwekezaji Uwekezaji huu ndani yake una mikono ya viongozi na watendaji walafi ambao hujificha katika kivuli cha wageni, huku wakiendelea kula nchi yao huku wakijidai kuwalalamikia wawekezaji kwa kutafuna rasilimali za taifa bila kuwasaidia wazawa. Leo hii maeneo mbalimbali yamebaki mashimo baada ya dhahabu au almasi kuchimbwa, lakini maisha ya wananchi yamebaki duni huku wakijisia kwa kujengewa vituo vya afya na vijumba visivyolingana na mali iliyovunwa na wawekezaji. Baadhi ya viongozi tulionao hivi sasa hawapitishi mradi husika au kumkaribisha mwekezaji bila ya watu kukatiwa fedha (ten pasenti). Cha kusikitisha zaidi hata hiyo miradi wanayopewa wawekezaji hao bado ni mzigo kwa taifa, kwa kuwa baadhi yao husamehewa kodi lakini pia wakati mwingine pia serikali huchukua fedha za walipa kodi kuisaidia miradi inayolegalega. Kampuni za kufua umeme za Richmond, IPTL na nyinginezo ambazo kila kukicha zilikuwa zikilipwa mamilioni ya fedha ni miongoni mwa uwekezaji wa kinyonyaji ambayo ni matunda ya rushwa waliyapewa watendaji wa serikali. Sitanyamaza kuwaonya viongozi na watendaji kuacha matendo ya kifisadi kwani huklo tuendako tutakuja kuwapiga kiberiti kama tunavyofanya kwa wezi wanaoiba kuku huku mitaani kwetu. Wananchi watafikia hatua hiyo kwa kuwa tunaona kila mafisadi wanapofikishwa mahakamani ni kama vile mashindano ya nani anamiliki kiasi gani au mali zake zina thamani gani. Mahakama ya Kisutu hivi sasa imekuwa ni sehemu ya kuwaumbua viongozi kwa mali walizozichuma, lakini pia sehemu ya kuwapa hasira wananchi hasa kwa kutambua uovu wa kujilimbikizia mali kunakofanywa na watu waliopewa dhamana ya kuzisimamia rasilimali za taifa. Sitanyamaza kwa vile sitapenda kuona machafuko yanayotokana na wananchi baada ya kuchoshwa na vitendo vya kifisadi, ndiyo maana nimeamua kuwaonya mapema watendaji na viongozi wa serikali ili tuendako tusije tukalaumiana kama alivyosema Rais Jkaya Kikwete, alipokuwa akitoa hotuba ya kuuaga mwaka 2008 na kuukaribisha 2009.

Salehe Mohamed
Tanzania Daima~Sauti ya watu

No comments: