February 17, 2009

ZOMBE AKALIWA KOONI

Mshitakiwa wa tatu, Ahmed Makelle, katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi, amedai aliyekuwa Kaimu Kamanda na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe, ni mwongo na alimbambikia kesi kutokana na maelezo ya uongo aliyoandika dhidi yake. Akitoa utetezi wake mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati, Makelle alidai kwamba maelezo ya Zombe ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, alimbambikia kesi kwamba alitoa taarifa kupita radio ya polisi kwamba majambazi yamepambana na polisi, wakati si kweli. Mshitakiwa huyo alidai kwamba alishuhudia watuhumiwa hao wakikamatwa wakiwa hai na kwamba hakukuwa na mapambano kati yao na askari polisi kama alivyodai Zombe kwenye maelezo ambayo aliyaruka mahakamani jana. Madai hayo yanapingana na yale yaliyotolewa ya Zombe, kuwa waliouawa walikuwa wakipambana na polisi kwenye ukuta wa Posta Sinza jijini Dar es Salaam. Alidai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa hata yeye alishangaa aliposikia taarifa kuwa watuhumiwa hao wameuawa wakati wakipambana na askari polisi. Jaji Massati alianza kusikiliza kesi hiyo mwaka jana wakati huo akiwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu na sasa anaendelea nayo licha ya kupanda kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Kesi hiyo inayomhusisha Zombe na wenzake tisa ilianza kunguruma tangu katikati ya mwaka 2006 ambapo jumla ya mashahidi 37 walitoa ushahidi wao mahakamani hapo. Makelle pia alidai mahakamani hapo kuwa Zombe aliandika maelezo ya uongo kuwa alimsikia yeye (Makelle) akitangaza katika redio call kuwa waliouawa walikuwa majambazi waliokuwa wakipambana na polisi. ``Hizo taarifa mtukufu Jaji ni za uongo mtupu na sijawahi kutoa maelezo hayo na huenda yaliandikwa na makao makuu, siyatambui,\" alidai mshitakiwa huyo. Makelle ambaye ni mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, alidai kuwa Zombe alipofika kituo cha Polisi cha Urafiki alikuwa mkali sana alipokuta fedha pungufu na kwamba hakuulizia kabisa kuhusu walipo watuhumiwa. Akiongozwa na wakili wa upande wa mashitaka, Mugaya Mutaki, Makelle, alidai kuwa baada ya askari wa kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwakamata watuhumiwa hao, aliwaamuru wapelekwe kituoni kwa mahojiano zaidi. Alidai watuhumiwa hao walipandishwa katika gari aina ya Pick Up ya polisi wakiwa hai, lakini baadaye alishangaa kuambiwa kuwa kuna majambazi wanne wamekufa wakati wakipambana na polisi. Mahojiano kati ya Mutaki na Makelle yalikuwa hivi: Mutaki: Ahmed Makelle tueleze kabla ya kukamatwa ulifanya kazi Jeshi la Polisi kwa muda gani? Makelle: Mtukufu Jaji nimefanya kazi kwa miaka 16. Mutaki: Ulikuwa kitengo cha upelelezi? Makelle: Ndiyo kule nilikuwa mtaalamu. Mutaki: Mtaalamu wa nini? Makelle: Mtaalamu wa maandishi. Mutaki: Ulifanya kazi hiyo kwa miaka mingapi? Makelle: Miaka 14. Mutaki: Uliwahi kufanya kazi kitengo cha utoaji wa vibali vya silaha? Makelle: Hapana sikuwahi kufanya kazi huko. Mutaki: Kitengo hicho si ndicho kinatunza kumbukumbu za silaha zinazomilikiwa kihalali? Makelle: Sijui kwa kuwa sijawahi kufanya kazi huko. Mutaki: Je, ukitaka kujua uhalali wa silaha unayoitilia shaka unaenda kitengo gani? Makelle: Central Armoury Register. Mutaki: Ukikamata silaha labda unataka kuihakiki si unaenda Central Armoury Register? Makelle: Ndiyo ukiitilia shaka unaenda kuihakiki huko. Mutaki: Je, majibu yanaweza kupatikana kwa muda gani? Makelle: Inategemea, unaweza kupata ndani ya wiki au pengine mwezi. Mutaki. Hivi inawezekana ukapata jibu ndani ya siku moja. Makelle: Si rahisi. Mutaki: Tarehe 14/1/2006 ulipata taarifa za tukio la Bidco kutoka OC 99 saa ngapi? Makelle: Saa 12 jioni. Mutaki: Namba yako ya radio call ni ngapi? Makelle: 158. Mutaki: Siku ulipopata taarifa za tukio unasema ulienda na askari, unaweza kuwataja ni nani na nani? Makelle: Koplo Jane na mshitakiwa wa kumi. Mutaki: Mlitumia usafiri gani kufika huko? Makelle: Saloon ndogo. Mutaki: Hilo gari ilikuwa mali ya nani? Makelle: Yangu. Mutaki: Unakumbuka ilikuwa na rangi gani? Makelle: Nyeupe. Mutaki: Ile ilikuwa gari yako bila shaka unaweza kukumbuka usajili wake. Makelle: Mtukufu Jaji nimesahau namba ila ilikuwa inaishia na herufu AAA. Mutaki: S[aloon aina gani vile? Makelle: Toyota Carina nyeupe. Mutaki: Unakumbuka mlibeba silaha zozote? Makelle: Ndiyo mimi nina bastola nilienda nayo. Mutaki: Je, hao askari wengine ulioenda nao walikuwa na silaha? Makelle: Hapana. Mutaki: Kutoka Urafiki mlielekea barabara ipi? Makelle: Barabara ya Morogoro kisha Shekilango. Mutaki: Mlienda hadi wapi? Makelle: Shule ya Msingi Mugabe kisha tutaingia kushoto. Mutaki: Mlipoingia kushoto mlienda mbele umbali gani? Makelle: Tulipita mtaa wa kwanza na wa pili tukakunja kulia kuna barabara ya vumbi. Mutaki: Hebu ieleze mahakama hii hapo mlikuta nini? Makelle: Kundi kubwa la watu na hiyo ilinifanya nihisi kuna kitu. Mutaki: Je, ulienda hapo? Makelle: Nilisogelea ila nilisimamishwa na askari namkumbuka alikuwa Koplo Nyangerela. Mutaki: Alikueleza kulikuwa na nini hapo? Makelle: Ndiyo alisema kuna gari wanalihisi hivyo wanalikagua. Mutaki: Kwa kuwa eneo lile ni eneo lako la kazi bila shaka utakuwa unafahamu pale panaitwaje? Makelle: Sikumbuki vizuri, lakini ninachojua pale ni Sinza. Mutaki: Unakumbuka mahakama ilitembelea maeneo ya Sinza na ukuta wa Posta, je, hapo ni moja ya maeneo ambapo mahakama ilitembelea? Makelle: Ni kama maeneo hayo. Mutaki: Si ndipo makazi ya Bernadeta na Mjatta? Makelle: Siwezi kujua? Mutaki: Kumbuka mahakama ilitembelea Sinza Palestina na Ukuta wa Posta, sasa hapo unaposema wewe ni wapi? Makelle: Ni pale ambapo mahakama ilisimama kwa mara ya kwanza. Mutaki: Hivi huyu Koplo Nangerela alikuwa na silaha? Makelle: Ndiyo alikuwa na SMG. Mutaki: Hatimaye watuhumiwa walikamatwa na wakapakiwa katika gari, wewe kama mtu uliyekuwa na cheo kikubwa kuliko askari wote waliokuwa pale ulifanya nini? Makelle: Niliamuru wapelekwe kituo cha polisi Chuo Kikuu kwa mahojiano zaidi. Mutaki: Walipokuwa wamepakiwa walikuwa na pingu? Makelle: Sikuona kama wana pingu. Mutaki: Ulielekeza wapelekwe wapi? Makelle: Kwa kuwa hawakuwa katika mamlaka yangu niliamuru wapelekwe kituo chao cha kazi ambacho ni Chuo Kikuu. Mutaki: Lakini inaonekana Urafiki ni karibu zaidi kwa nini uliamuru wapelekwe Chuo Kikuu? Makelle: Hapana, Urafiki ni mbali zaidi. Mutaki: Hivi kulikuwa na askari mwenye cheo zaidi yako? Makelle: Hapana. Mutaki: Vyeo uliwazidi sio? Makelle: Inawezekana. Mutaki: Ile Pick Up iliyowabeba wale washukiwa uliitambua ni ya wapi? Makelle: Ndiyo, niliitambua kuwa ni ya Chuo Kikuu kwa kuwa ilikuwa gari pekee ya polisi yenye namba SU. Mutaki: Hiyo Pick UP ilikuwa na rangi gani? Makelle: Blue. Mutaki: Je, ilikuwa na maandishi pembeni yanayoashiria kuwa gari hilo ni mali ya Jeshi la Polisi. Makelle: Hapana. Mutaki: Baada ya kuwapakia wale watuhumiwa waliwapeleka wapi? Makelle: Mimi niliwaelekeza wawapeleke kituoni Chuo Kikuu. Mutaki: Walipitia wapi? Makelle: Pale mahakama ilipopita wakati inaenda Sam Nujoma. Mutaki: Mbali na hilo gari lililowabeba watuhumiwa kulikuwa na kielelezo gani? Makelle: Walitaka kunipa mkoba wenye pesa, lakini nilikataa niliwaeleza waende nao. Mutaki: Begi lilikuwa na hela? Makelle: Ndiyo, na hela ndizo ziliwafanya polisi wawatilie mashaka baada ya kuona wanababaika. Mutaki: Ile bastola nayo ulikabidhiwa wewe? Makelle: Sikupewa chochote walichokamatwa, niliwaambia waende navyo. Mutaki: Hao watuhumiwa walikuwa wangapi? Makelle: Wanne. Mutaki: Walikuwa wakitumia gari gani? Makelle: Saloon Car dark bluu. Mutaki: Waliwachukua wale watuhumiwa pale wakiwa hai, kweli si kweli? Makelle: Ndiyo. Mutaki: Ulisikia taarifa yoyote kwamba wamepambana na polisi baada ya hapo? Makelle: Sikupata taarifa hiyo. Wakili Mutaki alimwonyesha Makelle kielelezo D 10 chenye maelezo ya ACP Zombe yanayodai kuwa yeye Zombe alimsikia Makelle akitangaza kwenye redio call kuwa kuna majambazi yameuawa yakipambana na polisi. Makelle aliyakana maelezo hayo akidai kuwa yalitungwa na Zombe kwa sababu anazojua yeye. Mutaki: Kuna kielelezo kiliandikwa kuwa ulitoa taarifa za kuuawa majambazi ina maana Zombe alikusingizia? Makelle: Kweli kabisa, Zombe alinisingizia sana. Mutaki: Kwani una ugomvi na Zombe? Makelle: Hapana, nashangaa kwa nini aliamua kufanya hivyo. Mutaki: Unasema hukutangaza katika redio call kuwa kuna majambazi yameuawa wakati yakipambana na polisi unaweza kutueleza ambacho ulisema? Makelle: Nilisema askari wamekamata watu wanne wakiwa na bastola moja na niliagiza wapelekwe kituoni kwa mahojiano zaidi. Mutaki: Sasa ilikuwaje vielelezo vikapelekwa sehemu nyingine ya wilaya na watuhumiwa wakapelekwa sehemu nyingine ya wilaya? Makelle: Sina maelezo. Mutaki: Ile gari iliyokamatwa ilikuwaje ikapelekwa Urafiki? Makelle: Hata mimi nilishangaa kwa nini ilifika pale. Mbali na Zombe washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Christopher Bageni, Ahmed Makelle, Jane Andrew na Emmanuel Mabula. Wengine ni Koplo Michael, D 2300 Abeneth, Koplo Rajabu, Rashid Lema na Festus Chenge. Katika kesi hiyo washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006, katika msitu wa Pande uliopo huko Mbezi Louis nje ya Jiji la Dar es Salaam, walimuua Ephraim Chigumbi. Katika shtaka la pili, ilidaiwa siku na mahali pa tukio la kwanza washtakiwa walimuua Sabinus Chigumbi. Katika shtaka la tatu na nne, siku ya tukio la kwanza na la pili, washtakiwa waliwaua Mathias Lukombe na Juma Ndugu. Kesi inaendelea leo kwa mshitakiwa wa tano ambaye ni mwanamke pekee katika kesi hiyo, Jane Andrew, ataanza kutoa utetezi wake mbele ya Jaji Massati.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22