Kwanini kisa hiki kimetokea?Hili ndilo swali kubwa hii leo kila mmoja analojiuliza kuhusiana na mauaji yaliyotokea katika shule ya Albertville katika eneo la Winnenden. Hata wanafunzi wa shule hiyo na wanafunzi wengine wanajiuliza swali hilo hilo, kwanini? Lakini polisi hadi sasa wanajaribu kubaini nini hasa lilikuwa lengo la mshambuliaji huyo.
Hali ya majonzi ilitanda asubuhi ya leo Alhamisi, waandishi wa habari walifika kwa wingi katika eneo hilo kushuhudia kinachoendelea ikiwa ni pamoja na shughuli za maombolezi.Mzazi mmoja alisema maneno haya yafuatayo kuhusu hisia zake katika kisa hiki.
''Najisikia vibaya sana, sijui hata nieleze nini, ni kama wazazi wengine watoto wangu wako katika hali nzuri lakini wale wahanga wa tukio hili ni kama watoto wangu, inaniumiza sana.''
Bila shaka, hakuna shughuli yoyote ya mafunzo itakayoendelea leo hii katika shule hiyo. Badala ya kuwa shuleni humo leo hii, wanafunzi wa shule wamekwenda katika jumba la wataalamu wa masuala ya kisaikolojia ambao wengine pia walitokea kutoka mikoa mingine ya Ujerumani na kuja hapo Winnenden kushughulikiwa na idara ya dharura ya shirika la msalaba mwekundu la Ujerumani,kama anavyofafanua afisa mmoja wa shirika hilo.
''Tunasaidiana sote kwa kuwaunga mkono wanafunzi hao na natumai kwamba tutaimudu siku ya leo pia. Leo tunatarajia wanafunzi kiasi ya 150 kuja shuleni na kuna wengine ambao watabakia majumbani. Bila shaka, leo haitokuwa siku ya kawaida ya shule, tunasubiri kuona jinsi mambo yatakavyokuwa.''
Maafisa wa upelelezi nchini Ujerumani wanasema kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 17 alifyatua risasi kwa kutumia bastola ndani ya madarasa katika shule ya Albertville ambako alikuwa ni mwanafunzi wa zamani na kuwauwa wanafunzi kadhaa kwa mpigo mmoja kabla ya kujiua mwenyewe kwa kujipiga risasi. Kwa jumla, aliwaua watu 15 katika tukio hilo la kushtua.
Kansela Angela Merkel hapo jana akizungumzia masikitiko yake juu ya tukio hilo alisema-
''Leo ni siku ya huzuni ujerumani nzima na mawazo yetu yako pamojka na familia za wahanga tunawafikiria na tunawaombea''
Hakuna ajuae nini lilikuwa lengo la mtu huyo, ingawa wengi wa wahanga walikuwa ni wasichana, wanafunzi tisa waliouwawa wanane kati yao walikuwa ni wasichana na hata waalimu wote watatu waliouwawa walikuwa wasichana.
Wanaume watatu waliuwawa baadae wakati mshambuliaji huyo akijaribu kutoroka.
Polisi wanasema huenda mshambuliaji huyo alichukua bastola hiyo kutoka nyumbani kwao kutoka hifadhi maalum ya silaha za babake ambaye alikuwa mwanachama wa kilabu kinachoruhusiwa kumiliki silaha.
Polisi hawajabaini lolote kuhusiana na lengo la mshambuliaji huyo aliyetambulika kama Tim K huku mijadala mbali mbali ikiendelea kuhusiana na tukio hilo la kusikitisha.
Hata hivyo, kitu kimoja ambacho bila shaka ni lazima kiwepo ni kurudi kwa hali ya kawaida katika eneo hilo la Winnnenden na hasa katika shule ya Albertville na maisha lazima yaendelee.
No comments:
Post a Comment