April 29, 2009

SIKU 100 ZA OBAMA WHITE HOUSE

MR.PRESIDENT OBAMA
Ni siku 100 tangu Barack Obama kuuanza kutimiza majukumu yake.Wengi walitaraji kwamba kwa sasa umaarufu wa kupata kiongozi mpya utakuwa umepungua ila wafuasi wake bado wanasherehekea tukio hilo la kihistoria.Hapa Ujerumani nako wengi ya wakazi wa nchi hii wanaamini kuwa anatimiza wajibu wake anavyopaswa.Baadhi ya mambo yanayoripotiwa kuwafurahisha wengi ni azma ya kuifunga jela ya Guantanamo iliyoko Cuba,kupiga marufuku mateso dhidi ya wafungwa ,kuondoa wanajeshi wake nchini Iarq pamoja na kuinyoshea mkono Iran.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameonyesha kwamba anafurahishwa na kiongozi mpya wa Marekani Barack Obama.Bibi Merkel amezipongeza juhudi zake za kutafuta ufumbuzi wa mtikisiko wa kiuchumi unaogubika ulimwengu mzima na kwamba analipa kipa umbele suala la ushirikiano na washirika wenzake ikiwemo Ujerumani.Hilo limesisitizwa na Jens Plötner msemaji wa serikali ya Ujerumani aliyesema''Katika siku hizi 100 za mwanzo sera za kigeni za Marekani zimefanyiwa mabadiliko mengi mazuri.Tumeshuhudia mikakati mingi mipya katika sekta nyingi ambazo zina manufaa kwa sera za nje za Ujerumani.Kuzuia ueneaji wa silaha za nuklia,hatua ya kuinyoshea Iran mkono pamoja na msukumo mkubwa zaidi katika mchakato mzima wa kusaka amani ya eneo la Mashariki ya Kati vilevile msisitizo wa kutaka kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa… yote hayo ni mambo ambayo Ujerumani inayapa uzito.Tunahisi kwamba Rais Obama ana nia ya kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi.''Wajerumani wengi wanaikumbuka vizuri hotuba ya Rais Obama alipozuru mji wa Berlin mwaka uliopita.Rais Obama alilakiwa na kukaribishwa kwa shangwe na nderemo. Mpaka sasa zikiwa ni siku 100 tangu ashike wadhifa huo wengi bado wanavutiwa na ucheshi wake,''Ni aina ya mwanasiasa tungependa kuwa naye katika eneo la Ulaya magharibi.Anatofautiana na Bush na hilo lina manufaa kwake.Bila shaka siku 100 hazitoshi kutathmini utendaji wake na kupitisha maamuzi.

Bibi mmoja mkazi wa Berlin aliongeza kuwa ''Ana mawazo mazuri ya kutaka kufanya mabadiliko.Ila nina wasiwasi huenda asifanikiwe kwasababu hali ya kiuchumi ni ngumu kwa sasa hivi na huwezi kufanya mabadiliko bila ushirikiano. Maoni kama hayo pia anayo msemaji wa mambo ya kigeni wa chama cha Liberal Free Demokratik Werner Hoyer.Yeye kadhalika amefurahishwa na utendaji wa Rais Obama mpaka sasa.''Nadhani anatimiza baadhi ya ahadi alizotoa.Mwanzoni Kulikuwa na mitazamo tofauti ikiwa kama ataweza kufanya hilo.Ukitathmini kasi anayokwenda nayo nadhani atafanikiwa.''Kwa upande mwengine wakosoaji wa Rais Obama ni wachache.Wengi wao wanahoji sera zinazohusiana na walioshtumiwa kuhusika katika vitendo vya mateso katika jela za CIA wakati wa utawala wa mtangulizi wake George Bush. Mwanasiasa wa ngazi za juu katika chama cha Kijani Jürgen Trittin anakubaliana na mawazo hayo lakini anaongeza kuwa utendaji wa Rais Obama katika kipindi cha siku 100 za mwanzo ni mzuri.,''Amelipa bara la Ulaya vilevile serikali ya Ujerumani changamoto hususan katika azma yake ya kusitisha matumizi ya silaha za nuklia kote ulimwenguni.Kadhalika amezipa changamoto nchi zinazopinga juhudi za Uturuki za kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa kuinga mkono.Pia ameleta uhai mpya katika uhusiano kati ya Marekani na bara la Asia.Kwahiyo nadhani huu ni mwanzo mpya kwa kweli''

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22