May 22, 2009

Barack Obama kuibadili sura ya Marekani katika ulimwengu wa Kiarabu.

Rais wa Marekani Barack Obama ana fursa nzuri kuibadili sura ya Marekani katika ulimwengu wa kiarabu, lakini hata hivyo ana muda mfupi wa kufanya hivyo kulingana na maoni kutoka kwa umma yaliyotokana na utafiti uliofanywa katika nchi za Misri, Jordan, Lebanon,Morocco, Saudi Arabia pamoja na miliki ya nchi za kiarabu.
Utafiti huo uliotolewa siku ya jumannne ulionyesha kuwa asilimia arobaini na tano ya waarabu wote elfu nne waliohojiwa katika mataifa matano, wana hisia nzuri juu ya rais Barack Obama kinyume na asilimia ishirini na nne walio na hisia tofauti.
Hata hivyo hisia dhidi ya sera za marekani katika ulimwengu wa kiarabu zilionekana kubadilika kwa karibu mwaka mmoja uliopita, wakati hisia juu ya marekani na dhidi ya rais wa Zamani George Bush zikiwa mbaya zaidi.
Utafiti wa sasa ulionyesha uungwaji mkono kwa rais Barack Obama pamoja na Marekani huku asilimia sabini na nne ya nchi za kiarabu, zikiunga mkono kuundwa kwa taifa la palestina hali kadhalika zikionyesha huruma wao dhidi ya kundi la Hamas kuliko kundi la Fatah.
Watatu kati ya waarabu wanne wanaunga mkono kuundwa kwa mataifa mawili ya Israel na palestina, kama njia ya kumaliza mgogoro uliopo kati ya pande hizo mbili lakini hata hivyo kati ya walio hojiwa wanaamini kuwa ni vigumu kufikiwa kwa makubaliano ya amani.
Utafiti huo pia uligundua kuongezeka kwa hisia dhidi ya mipango ya nuklia ya Iran na kupungua kwa umaarufu wa kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah hasa nchini Misri na Morocco .
Utafiti huo unafanyika wakati kukiwa na shughuli nyingi za kidiplomasia zinazofanywa na utawala wa rais Obama, baada ya kumteua George Mitchel kama mjumbe wa amani katika ulimwengu wa kiarabu na Israel. Hadi sasa mitchel ameshafanya ziara tatu katika eneo hilo tangu ateuliwe na ana mipango ya kuweka ofisi yake mjini Jerusalem.
Wiki iliyopita rais Barack Obama alimualika katika ikulu ya Marekani mfalme Abdullah wa Jordan na pia kukutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumatatu. Wiki ijayo rais Obama anatarajiwa kukutana na rais wa mamlaka ya palestina mahmoud Abbas baada ya rais wa Misri Hosni Mubarak kuhairisha ziara yake nchini Marekani.
Juni nne mwaka huu rais Obama anatarajiwa kuhutubia ulimwengu wa kiarabu kutoka mji wa Cairo nchini Misri, katika kile kinachoonekana kama kinyume na sera za mtangulizi wake kuhusu vita dhidi ya ugaidi suala ambalo waislamu wengi waliliona kama vita dhidi ya uislamu.
Hotuba ya rais Obama pia inatarajiwa kugusia lengo la utawala mpya nchini Marekani la kupatikana kwa amani mashariki ya kati kama njia muhimu ya kuimarisha uhusiano katika ya marekani na ulimwengu wa kiarabu.
Utafiti wa hivi majuzi ulionyesha kuwa hata kama bado kuna shaka kuhusu mipango ya Marekani katika eneo la mashariki ya kati, kuchaguliwa kwa Obama na miezi ya kwanza uongozini huenda kukabadili mawazo mengi.
Wengi wa waliohojiwa, asilimia arobaini na sita walisema kuwa, wangependa wanajeshi wa Marekani waondoke nchini Iraq huku asilimia 26 wakitaka kusuluhishwa kwa mzozo uliopo katika ya Waisrael na wapalestina.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22