May 19, 2009

Mtuhumiwa wa wizi Dar auawa na kuchomwa moto

Mtu mmoja ambaye hakuweza kufahamika jinsia yake wala umri wake, amefariki dunia kwa kupigwa kisha kuchomwa moto na watu wasiofahamika kwa tuhuma za wizi. Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa ILala, Aibula Tanda amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo, majira ya saa 9:00 katika maeneo ya Buguruni Bonde la Tabata. Kamanda Tanda amesema mtu huyo hakuweza kutambuliwa kwa kuwa mwili wake ulikuwa umeteketezwa vibaya na kubaki majivu. 

Aidha amesema hadi sasa haijafahamika mtu huyo alidakwa akiiba nini na kwa nani.Amesema mabaki ya mwili huo yamehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Amana na hakuna anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo. 

Wakati huo huo, masalia ya mtu wa jinsia ya kiume ambaye hafahamiki yameokotwa huko maeneo ya Makongo, Jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mark Karunguyeye amesema masalia hayo yaliokotwa jana majira ya saa 8:00 mchana. 

Akasema mabaki hayo yamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi

No comments: