Askari mmoja wa Usalama barabarani (trafiki) yamemkuta makubwa leo asubuhi pale katika taa za kuongozea magari Ubungo Jijini baada ya kuvamiwa wakati akiwa kazini na kupewa kichapo kwa tuhuma za kuzipendelea gari za upande mmoja.
Tukio hilo limetokea kwenye eneo hilo la makutano ya barabara za Sam Nujoma, Morogoro na Mandela.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa watu waliompa kipigo askari huyo ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ.
Akisimulia tukio hilo, shuhuda mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, amesema maafande hao wa JWTZ walikuwa kwenye msafara wa magari manne, wakitokea maeneo ya Mwenge kuelekea Buguruni.
Akasema msafara huo ambao ulitanguliwa na gari moja dogo aina ya Landrover Defender na kufuatiwa na mabasi makubwa matatu, ulipofika kwenye mataa ya Ubungo ulisimama kama ilivyokuwa kwa magari mengine ya kiraia na kusubiri kuruhusiwa kupita.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, magari hayo ya JWTZ yalisimama kwa muda mrefu kusubiri, wakati traffiki aliyekuwa akiongoza magari mahali hapo akiwa 'bize' kuruhusu magari yanayokwenda na kutoka mjini kwa kutumia barabara ya Morogoro.
Akasema baada ya askari wa JWTZ kuona hivyo, baadhi yao waliteremka kwenye gari na kumfuata trafiki huyo.
Akasema askari hao wa JWTZ wakazungumza na afande mwenzao wa usalama barabarani kwa namna ambayo ilidhaniwa kuwa ni ya kumsihi awaruhusu kupita, kwani baada ya kuteta naye walirejea kwenye gari lao na kuendelea kusubiri.
"Zikapita tena dakika kadhaa... trafiki akaendelea kuita magari ya barabara ya Morogoro na ghafla, tukaona baadhi ya wanajeshi wakishuka tena na kumwendea trafiki," akasema shuhuda huyo.
Akasema walipomfikia, walizungumza tena kwa mara ya pili na wakarudi tena kwenye magari yao na kuendelea kusubiri.
Hata hivyo, akasema trafiki huyo aliyekuwa akiongoza magari akaendelea na utaratibu wake kama kawaida, huku gari za barabara ya Mandela na Sam Nujoma kulikokuwa na wanajeshi zikiendelea kusubiri.
Akasema baadaye, ndipo wanajeshi waliposhuka tena garini kwa mara ya tatu na kwenda kuchukua jukumu la kuongoza magari wenyewe.
"Baada ya hapo, tukaona wanajeshi kama wanne hivi wakishuka kwenye gari moja na kumfuata trafiki. Mmoja alipofika, akanyoosha mkono kuzuia magari ya barabara ya Morogoro huku trafiki naye akizidi kuyaruhusu... hapo ndipo wanajeshi wakamgeukia na kuanza kumpiga vibao," akasema shuhuda huyo.
Akasema kuwa wanajeshi hao walipomdhibiti trafiki huyo na kuwashangaza watu kwa kumuadhibu kwa makofi, baadaye wakapitisha msafara wao na kumfanya yule trafiki alazimike kuondoka eneo hilo kwa huzuni.
"Badaye, magari ikabidi yaendelee kuongozwa na taa kwa sababu yule trafiki naye aliondoka," akasema shuhuda huyo.
Hadi Alasiri inaondoka kwenye eneo hilo, magari yalikuwa yakiongozwa na taa za barabarani na askari wawili wa usalama barabarani walionekana wakirandaranda katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment