September 15, 2009

Wachache kuiona Miss Tanzania


Kamati ya mashindano ya Miss Tanzania imeteua kampuni mbili za hapa nchini kwa ajili ya kuuza tiketi kwa wadau watakaofika kuhudhuria onyesho la Vodacom Miss Tanzania mwaka huu ambalo limepangwa kufanyika Oktoba 2 kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Mawakala hao walioteuliwa ni Jambo Concepts Tanzania Limited na Massive Company Limited. Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga alisema kuwa wameamua kuteua kampuni hizo mbili kutokana na ukumbi ambao shindano hilo linafanyika kuingiza watu wachache ukilinganisha na kumbi nyingine zilizofanyikia shindano hilo. Lundenga alisema kuwa ukumbi huo wa Mlimani City unauwezo wa kuingia mashabiki 3,500 wakati kwenye eneo la viwanja vya Leaders watu walikuwa wanafikia 6,500 au zaidi. Alisema kuwa kiingilio cha juu mwaka huu ni Sh. 100,000 katika eneo litakalojulikana kana Platinum na sehemu nyingine ya dhahabu wadau hao watalazimika kulipa kiasi cha Sh. 50,000."Hatutarajii kuuza tiketi zaidi ya idadi hiyo na tunawaomba wadau wa mashindano ya urembo kununua mapema tiketi kwa ajili ya kuepuka usumbufu," alisema Lundenga. Alisema pia hata mandhari ya ukaaji katika shindano hilo yameboreshwa na yatakuwa na hadhi ya kimataifa tofauti na miaka iliyopita. Jumla ya warembo 30 kutoka kanda 10 za hapa nchini wamefanikiwa kufika fainali hizo ambapo zinadhaminiwa na Vodacom, Redd's, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), TANAPA, Hifadhi ya Ngorongoro, Samsung, ATC, Giraffe Ocean View Hotel, TBC na New Habari 2006.

Warembo wanaowania taji hilo jana walikuwa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuelezwa mambo mbalimbali yanayohusu Mlima Kilimanjaro na leo wanatarajia kuelekea Arusha kutembelea vivutio vya utalii.

No comments: