February 10, 2010

Mtanzania `Face of Africa` arejea

Kisura wa Tanzania Lilian Mduda

Kisura wa Tanzania Lilian Mduda. amerejea jana baada ya kumaliza ndani ya 10 bora ya mashindano ya ‘M-Net Face of Africa’ ambapo Lukundo Nalungwe wa Zambia aliibuka mshindi na kutwaa zawadi ya kwanza ya dola za Kimarekani 50,000 (sawa na Sh. Milioni 67).

Lilian hakuweza kuingia katika tano bora ya fainali za mashindano hayo yaliyofanyika juzi usiku katika hoteli ya Eko jijini Lagos, Nigeria, lakini alimaliza akiwa miongoni mwa visura kumi bora na hivyo kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

“Kwakweli Lilian hakutuangusha… amejitahidi sana na tunapaswa kumpongeza kwa hatua aliyofikia ambayo imetuletea heshima ya pekee,” alisema Furaha Samalu, Afisa Uhusiano wa kampuni ya Multi Choice kwa upande wa Tanzania. Multi Choice huandaa mashindano hayo kila mwaka.

Furaha alisema kuwa kisura Lilian, anayesomea shahada ya biashara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alitunukiwa zawadi kadhaa kwa kuweza kufika fainali na tayari amesharejea nchini.

Lukundo, 22, alitwaa taji hilo akiwashinda Lilian na visura wengine nane waliotinga fainali za michuano hiyo ambayo awali ilihusisha visura zaidi ya 400 kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika.

“Namshukuru Mungu na Wazambia wote kwa kuwa nami katika sala zao,” alisema Lukundo mara baada ya kutangazwa mshindi.

“Kuna wasichana wengi sana ambao wangeweza kuwa washindi na kwa kila mmoja aliyeniunga mkono, nasema asanteni… nimetunukiwa,” alisema kisura huyo, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu cha ZICAS mjini Kabwe, Zambia.

Kwa ushindi huo, Lukundo alitunukiwa zawadi ya fedha na pia alipata fursa ya kwenda Marekani wiki ijayo kwa ajili ya kushiriki maonyesho ya mitindo jijini New York.

Benki ya Zenith pia ilimzawadia dola za Kimarekani 5,000 ambazo ni sawa na Sh. Milioni 6.7.

No comments: