February 22, 2010

WARUSHA NDEGE LUFTHANSA WAGOMA

Shirika la Ndege la Ujerumani, Lufthansa limeripoti kuwa marubani wake wameanza mgomo wao wa siku nne. Chama cha marubani hao, Cockpit, awali kilikuwa kimekubali kukutana na Mkuu wa shirika hilo la ndege, lakini kikakatalia mbali masharti ya awali yaliyowekwa na usimamizi wa shirika hilo. Marubani hao 4,000 wanaitisha nyongeza ya asili mia sita, pamoja na uhakika wa ajira. Mgomo huo sasa unamanisha kutakuwa na msongamano wa abiria huku safari nyingi za ndege Barani Ulaya, zikicheleweshwa. Lufthansa inatarajiwa kufutilia mbali safari 800 za ndege kila siku, au theluthi mbili za ratiba yake. Waziri wa Usafiri wa Ujerumani Peter Ramsauer ameonya kuwa mgomo huo utaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa Ujerumani na amejitolea kuwa mpatanishi wa mzozo huo wa malipo. Shirika hilo la ndege la Lufthansa, limesema mgomo huo ambao ndio mkubwa kabisa katika historia ya shirika hilo, utagharimu zaidi ya Euro milioni 65.

No comments: