Kiasi cha wanajeshi 600 kutoka nchi za kigeni walipewa mafunzo mwaka jana na Bundeswehr,Jeshi la Ujerumani, humu nchini. Miongoni mwa nchi walikotokea wanajeshi hao ni Ethiopia, Nigeria, Kenya na hata Tanzania.
Kwa mwaka huu 2010,Ujerumani imeahidi kutoa msaada zaidi wa mafunzo ya kijeshi na kwa mujibu wa serikali ya Ujerumani, lengo ni kuwa kutokana na ushirikiano wa aina hii, wanajeshi hao wanaelimishwa sheria na demokrasia.
Kuwa mpango huu, sio kila mara unazaa matunda mema, tuna mfano wa Jamhuri ya Guinea, huko Afrika ya magharibi. Kwani huko hapo Septemba mwaka uliopita 2009, mwanajeshi wa miavuli aliepatiwa mafunzo Ujerumani alipata umaarufu wa kusikitisha: Wanajeshi wa Mtawala wa kijeshi Moussa Dadis Camara waliwafyatulia risasi na kuwaua waandamanaji kadhaa walioandamana kwa amani. Zaidi ya waandamanaji 150 wakauwawa.
"Mapinduzi ya kijeshi ya Wajerumani"-hivyo ndivyo njama ya mapinduzi ya Moussa Camara nchini Guinea, ilivyoitwa na baadhi ya watu. Nembo yake: kofia nyekundu yenye alama ya askari wa miavuli wa kijerumani. Moussa Camara alijipatia sifa zake barabara, kwani alihitimu mafunzo ya kijeshi ya miaka 4 nchini Ujerumani. Hata wanajeshi wengine wengi walioshiriki katika mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea, walipata mafunzo yao kutoka Bundeswehr, jeshi la Ujerumani.Waziri wa fedha, Mamadou Sande, au waziri wa ulinzi, Mamadouba Camara, ni miongoni mwao waliopata mafunzo Ujerumani.
Pale utawala huo wa kijeshi ulipoufyatulia risasi umma wake, Bundeswehr, jeshi la Ujerumani, likakomesha ushirikiano wa miaka mingi na Jeshi la Guinea. Februari, mwakani 2011, mwanajeshi wa mwisho wa Guinea ataihama Ujerumani. Na kuhusu mkasa wa Guinea, huo umekuwa uamuzi barabara, kwa mujibu asemavyo Thomas Silberhorn, msemaji wa maswali ya ulinzi wa chama cha CSU katika Bunge la Ujerumani-Bundestag. Kimsingi, anaunga mkono kutolewa mafunzo ya kijeshi kama chombo cha kuendeleza mbele demokrasia na kuilinda. Anasema:
"Msaada wa mafunzo ya kijeshi una shabaha ya kuimarisha uhusiano na nchi nyengine na kukuza kwa njia hiyo maadili ya kidemokrasia. Na hilo, kimsingi, ni jambo la kukaribishwa. Ni mafunzo ya kijeshi yanayofuatana na maadili tunayoyathamini nchini Ujerumani. Isitokee lakini, msaada huo wa mafunzo ya kijeshi ukaenda kinyume na maadili ya kuendeleza mbele demokrasia."
Kwa jumla, Bundeswehr, jeshi la Ujerumani, limeshirikiana mnamo miaka 10 iliopita na majeshi ya nchi 27 za kiafrika na kutoa mafunzo kwa viongozi wa kijeshi 1.200. Mradi huo unaandaliwa na kugharimiwa na wizara ya nje na ya ulinzi ya Ujerumani. Jinsi gani jeshi katika nchi shirika linastahiki kuwa mshirika na Bundeswehr, hakuna alie tayari katika mojawapo ya wizara hizo mbili kusimulia. Kumetolewa msaada wa mafunzo ya kijeshi kwa wanajeshi kutoka Ethiopia, Nigeria na Niger.
Kwa muujibu wa Bw.Mathias John wa Shirika linalotetea haki za binadamu ulimwenguni (Amnesty International), imesadifu kuwa ni majeshi yanayokanyaga haki za binadamu. Kwa hivyo, anadai kuwapo uwazi katika kutoa misaada hiyo ya mafunzo ya kijeshi.
No comments:
Post a Comment