October 03, 2010

MIAKA 20 TANGU UJERUMANI KUUNGANA TENA


Miaka 20 ni kama kupwesa na kupwesua tu kihistoria. Ndipo mtu anaweza kufikia katika kipindi hiki cha miaka 20 cha kuunganishwa tena kwa Ujerumani. Lipi la kulalamikiwa na la kusifiwa?


Katika maadhimisho, huwa zinatawala takwimu: tarakimu na hesabu, za vile ambavyo sasa Ujerumani imekuwa baada ya miaka 20 ya kuunganishwa tena. Na hilo ni jambo la kweli: nyingi kati ya takwimu hizi zinaonesha kwamba ndani ya miongo hii miwili iliyopita, yamefanyika makosa pia, kwamba kumekuwa bado na ukosefu wa uadilifu, kwamba kiwango cha ukosefu wa kazi Mashariki kinapindukia mara mbili ya kile cha Magharibi, kwamba watu wa Magharibi wanalipwa mshahara mkubwa zaidi kwa kazi ile ile wanayofanya watu wa Mashariki. Yote hayo mtu anaweza kuyasoma kwenye tafiti mbalimbali, lakini nini kinasemwa kuhusu Ujerumani yenyewe na Muungano huu? Si mengi.

Kihistoria ni Jambo la Kipekee

Mradi mkubwa na ambao bado haujakamilika wa historia ya Ujerumani baada ya vita hauwezi kuelezeka kwenye takwimu tu. Bila ya shaka wabunge wa zamani wa Magharibi wanauhisi ule mzigo wa kifedha, ambapo milioni za Euro zilipelekwa Mashariki kutoka kwao na bado kuna nyengine zinahitaji kupelekwa. Bali bado kubwa zaidi ya yote ni changamoto linalowakabili watu wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki, ambao baada ya kuishi miaka kadhaa chini ya mfumo wa dola kuhodhi mambo yote ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, sasa wanalazimika kuishi katika maisha mapya.

Bila ya shaka mafanikio yanayoonekana kwenye jamii ya Kijerumani hayawezi bado kuthibitishwa. Pande zote mbili, Mashariki na Magharibi, kuna mengi ya kulalamikiwa, baadhi ya malalamiko ni ya haki na mengine porojo tu za kisiasa. Kwa kuwa si jambo linalowezekana kuwa na jamii mbili ambazo zimeinukia kutoka historia na tabia tafauti, zikae kwa miongo miwili mizima bila ya kuwepo kwa malalamiko. Yule ambaye leo, baada ya miaka 20, anapuuzia kuwepo kwa tafauti baina ya Mashariki na Magharibi, huyo atakuwa hakuzingatia vigezo halali kwenye uchambuzi wake.

Hakukuwa na Wakati wa Kufanya Majaribio

Lakini hakuna linaloweza kubadilisha ukweli, kwamba baina ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na tarehe 3 Oktoba 1990, Ujerumani ilipoungana tena, palifanyika makosa mengi na mambo mengi yaliangaliwa sivyo. Lililopo wazi ni kuwa, wabunifu wa muungano wa Ujerumani wakati huo hawakuwa na muda wa kufanya majaribio kwanza, wala hawakuwa na muda wa kulipeleka suala la umoja wa Wajerumani kwa mwendo wa taratbu. Walilazimika kuitumia fursa ya kihistoria iliyojitokeza kufanya mabadiliko haya makubwa - na ndivyo walivyofanya.

Kuna ambao wanaona kwamba kama jambo hili lingefanywa taratibu, kwa kuzungumza na watu kwanza, muungano huu ungechukua muda na gharama ndogo zaidi kuwezekana, kuliko alivyofanya Chansela wa wakati huo wa Ujerumani, Helmut Kohl. Lakini sentensi hizi ni silaha nyepesi zinazotumiwa na wakosoaji wa Kohl kwenye midahalo na majadiliano.

Si hoja za msingi, kwa sababu ukweli ni kuwa licha ya yote, kila mmoja amenufaika na heshima iliyoletwa na Muungano huu. Miongoni mwa manufaa hayo ni kuwa katika miaka hii 20 iliyopita tumekuwa wawazi zaidi, mchanganyiko zaidi, na watulivu zaidi. Tumejifunza kwamba ili kutatua migogoro inayoibuka kwenye jamii zetu, ni lazima kutafuta majibu ya masuali yanayoibuliwa na migogoro hiyo kwa uwazi na sio kuyakumbiza masuali hayo chini ya zulia. Hakuna tena haja ya kutafuta lililofichwa chini ya kilemba ikiwa sasa tunaweza kuliona mbele ya macho yetu.

Ujerumani sasa ni maabara, ambayo kwayo jamii ya Ulaya, wanaweza kupima na kujifunza namna mabadiliko, changamioto na uzoefu mpya lazima vichanganywe na viende pamoja. Hiyo nayo ni faida kubwa ya Muungano huu. Nayo inasema mengi kuhusiana na nchi hii kuliko takwimu.

CHANZO.DW-BONN

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22