November 11, 2010

Kesi ya Ghailani yaendelea kusikilizwa mjini New York

Ahmed Khalfan Ghailani.

Wakili wa Ghailani azisuta hoja za upande wa mashtaka na kuhoji mteja wake hakuwa akijua chochote kuhusu mashambulio ya kigaidi ya mwaka 1998


Mawakili wa Mtanzania Ahmed Khalfan Ghailani, anaetuhumiwa kushiriki katika mashambulio dhidi ya balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mnamo mwaka 1998 wanahoji mtuhumiwa huyo hana hatia.

Mnamo siku ya pili ya kusikilizwa hoja za mwisho mwisho katika kesi hiyo, iliyoanza kusikilizwa October 12 mwaka huu,wakili Peter Quijano amehakikisha kwamba mteja wake "hakuwa akijua chochote na kwamba alidanganywa."

Wakili huyo amekosoa pia ushahidi uliotolewa na serikali, akisema "ni dhaifu na wa kutiliwa shaka."

Amekanusha pia hoja kwamba Ghailani alikwenda Pakistan kabla ya mashambulio hayo kutokea.

"Ingekua Ahmed alikuwa ndani ya ndege iliyokuwa ikielekea Pakistan, mngemsikia japo shahidi mmoja. Hakujakuwa na hata mmoja. Ahmed hajakuwemo ndani ya ndege hiyo na nyaraka zilizotolewa ni za bandia." Ameshadidia wakili Peter Quijano.

Mashambulio ya Agosti saba mwaka 1998 dhidi ya ofisi za ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya yaligharimu maisha ya watu 224 na zaidi ya 5000 kujeruhiwa.

Mwenyewe mtuhumiwa, Ahmed Khalfan Ghailani, mwenye umri wa miaka 36 hivi sasa, alikuwepo katika ukumbi wa mahakama akivalia shati rangi ya buluu na tai ya rangi hiyo hiyo.

Anatupiwa lawama ya kuhusika na visa 286 vya uhalifu, ikiwa ni pamoja na "njama ya kutaka kuwauwa Wamarekani."

Wakili wa upande wa mashtaka, Michael Farbiarz, anasema "hoja hizo hazina msingi." Anasema:" Siku ya mashambulio, Ahmed Ghailani aliacha kila kitu alichokuwa nacho maishani mwake, marafiki zake, familia yake, kazi yake na jina lake. Ghailani ni muongo, hakuna maana kwa hivyo kudai amedanganywa."

Wadadisi wanajiuliza kama kisheria ni sawa kesi hiyo kusikilizwa nchini Marekani katika wakati ambapo mashambulio yametokea Afrika mashariki.

Baada ya kusikilizwa hoja za pande zote mbili, na jaji Lewis Kaplan kutoa neno lake, jopo la majaji litaanza kushauriana hii leo.

Chanzo.DW-Bonn

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22