January 25, 2011

Simu za Mkononi Kuokoa Maisha ya Mama Wajawazito

Hospitali ya Uzazi ya Pumwani, katika kitongoji maskini cha Eastlands jijini Nairobi, ni eneo la mradi wa majaribio kwa kutumia simu za mkononi kusaidia mama wanaoishi na VVU kuzuia kuambukiza watoto wao virusi hivyo.

Juliet Wangari Njuguna ni nesi mtafiti katika Mradi wa Kudhibiti UKIMWI Kenya. Anafanya kazi katika kliniki ya Pumwani kusaidia mama wanaoishi na VVU.

"Tunasaidia na kuwajali, na wakati wagonjwa wakija tunawatenganisha. Tumeongea na wale ambao walikuwa na VVU, na kutaka kujua ni kwa muda gani wamejua hali yao na kama wamewahi kumwambia mtu yoyote."

Pia wanataka kujua kama wanawake hao wana simu za mkononi.

Mwezi Julai, Mradi wa Kudhibiti UKIMWI Kenya ulianza kutumia Hospitali ya Pumwani kama kituo cha utafiti kujua jinsi ya kufuatilia wagonjwa wanaoishi na VVU kwa kutumia simu zao za mkononi.

Mawasiliano ya simu yana nia ya kuhakikisha kuwa mama wanaendelea kutumia madawa ya kurefusha maisha na kuwa na taarifa ya nini cha kufanya wakati wa mimba kupunguza hatari ya kuambukiza virusi kwa watoto wao.

Simu za mkononi zimekuwa njia muhimu ya kuwasiliana nchini Kenya. Kupungua kwa gharama kwa hivi karibuni kunakofanywa na watoaji huduma za simu kumehamasisha watu wengi zaidi kutumia simu za mkononi.

Daktari wa watoto, Frida Govedi, Ofisa Mtendaji Mkuu katika Hospitali ya Wazazi ya Pumwani, anasema, "kupitia simu za mkononi wanapewa uwezo wa kuwa na taarifa. Jinsi ya kula, ni lini wanatakiwa kutumia vidonge vya vitamini, ni lini wanapaswa kuja kupima kiasi cha CD4, ni njia ya masiliano ya pande mbili kati ya mama na mfanyakazi wa afya."

Njuguna na manesi wengi wa utafiti katika Hospitali ya Pumwani wanaongoza mama wenye VVU katika kliniki kupitia hojaji kujua kama wanahusika katika mpango wa simu za mkononi. Hojaji hurikodi taarifa za kina kama vile umri, afya yake kwa ujumla, ni kwa muda gani amejitambua kuwa na VVU na kama yuko tayari kuanza kutumia dawa yoyote.

Mama pia inambidi kuishi katika umbali ambao siyo mrefu sana kutoka hospitali na kuelewa vema lugha ya Kiingereza au Kiswahili. Majibu katika hojaji huingizwa kwenye databezi. Wanawake wote watapatiwa madawa ya kurefusha maisha, lakini kikundi kinachochaguliwa bila kuzingatia mpangilio wowote pia kitatumiwa ujumbe mfupi.

Wanawake wote watafuatiliwa baada ya kujifungua kujua mafanikio ya tiba. Hii pia ina lengo la kupima ufanisi wa ujumbe wa simu kwa mama wanaopokea ujumbe huo dhidi ya kundi ambalo halipatiwi ujumbe wowote.

"Wanawake wanaanza kupata ujumbe mmoja kwa wiki kukumbusha kuja kuhudhuria kliniki," anasema Njuguna. "Halafu katika mwezi wao wa mwisho wa mimba, ujumbe unabadilika kuwakumbusha kutumia madawa.

Lakini tunaandika, 'Kumbuka kutumia vitamini zako.' Hatutaki kuingiza 'ARVs' katika ujumbe mfupi, kwasababu hatujui ni nani atakuja kutumia simu yake." Njuguna anasema unyanyapaa na shinikizo la kuficha kujulikana kama mtu ana VVU ni changamoto kubwa kwa wanawake wanaoishi na VVU.

Umaskini uliokithiri ni changamoto nyingine, huku mara nyingine wanawake wakishindwa kuhudhuria miadi yao kutokana na kukosa pesa za usafiri au wakati mwingine kushindwa kufika kutokana na kufanya shughuli za kuwapatia pesa za matumizi.

Kutokujua kusoma na kuandika ni kikwazo kingine. "Jambo jingine ni kwamba baadhi yao wanajua Kiingereza na Kiswahili, lakini hawajui kusoma, na hivyo ujumbe wa simu hauwasaidii. Hivyo kuna baadhi ambao wanahisi kuwa afadhali kupiga simu siku zijazo."

Govedi ana wasiwasi kuwa faida za ujumbe wa simu ni kidogo kwa wale waliochelewa kujiunga katika mpango huo, ambao walikuwa na mimba kubwa wakati walipokuja Pumwani.

"Tungependa kuwapata mapema katika wiki ya 14, wakati tuna uwezo wa kutumia madawa ya kurefusha maisha kwa lengo la PMTCT. Lakini unakuta wengi wa mama hao wanakuja kwetu baada ya wiki ya 20," anasema Govedi.

Siku moja katika maisha ya wafanyakazi wa afya kutoa msaada kwa kutumia simu za mkononi ina kazi nyingi.

Njuguna lazima aendelee kujibu ujumbe wa simu na miito ya simu kutoka kwa zaidi ya wanawake 90 ambao wapo katika mpango huo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba taarifa muhimu zinapelekwa kwa wakati unaofaa.

Ujumbe wa kila mara umeingizwa kwenye kompyuta na kupelekwa automatiki, lakini wakati mfumo huo unapokuwa haufanyi kazi, mfanyakazi wa afya lazima kupeleka ujumbe huo kwa njia ya mkono kwa wanawake ambao wanategemea kukumbushwa.

Anahisi ni kazi ya nyongeza. "Ninajisikia vizuri tu kwamba unafanya jambo na wanalifurahia. Halafu wanauliza kila aina ya maswali, ambalo ni jambo zuri kuliko kuwa nyumbani na kubuni tu mambo. Hivyo unahisi kwamba unaleta mabadiliko katika maisha ya watu."

Mpango unatarajiwa kufikia mwisho katikati mwa mwaka 2013. Watafiti wanatarajia kupata matokeo chanya katika kuwapatia wanawake wanaoshi na VVU uwezo kulinda afya zao na afya za watoto wao wanaozaliwa.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22