January 07, 2011

Ujerumani yakumbwa na kashfa ya sumu kwenye chakula

Waziri wa Udhibiti wa Usalama wa Chakula wa Ujerumani, Illse Aigner

Takribani mabanda 1000 ya kufugia kuku wa nyama na mayai yamefungwa nchini Ujerumani baada ya mabaki ya dizeli, Dioxin, kugunduliwa katika chakula cha kuku.

Waziri wa Udhibiti na Usalama wa Chakula wa Ujerumani, Ilse Aigner, amesema kwamba hali ni mbaya, na serikali imelazimika kuyafunga mabanda hayo ili kuepusha uwezekano wa kuwaathiri watumiaji kiafya. Mabanda hayo, ambayo nchini Ujerumani yanaitwa mashamba, yamefungwa kufuatia kugunduliwa dawa hiyo iliyobainika kuwa na sumu.

Dawa hiyo inayotokana na mabaki ya dizeli imetumiwa katika kutengeneza chakula cha kuku wa nyama na mayai.

Kwa mujibu wa taarifa za idara zinazohusika karibu tani 3000 za chakula cha kuku zimeathirika na dawa hiyo yenye sumu.

Waziri wa kilimo bibi Ilse Aigner amesema hali ni mbaya na ameyataka majimbo yaliyoathirika na mkasa huo yatoe taarifa iwapo mayai yenye sumu ya Dioxin yameuzwa kwa wananchi.

Waziri huyo ameyapinga madai kwamba sumu hiyo imeingia kwa bahati mbaya katika chakula cha kuku.

Mawaziri wa kilimo wa majimbo yote ya Ujerumani watakutana baadae mwezi huu kuzijadili athari zilizosababishwa na dawa hiyo ya Dioxin.

Waziri wa kilimo wa jimbo la Thuringia J├╝rgen Reinholz amesema lazima adhabu kali itolewe kwa wote wanaovunja sheria za uzalishaji wa chakula cha mifugo. Amesema kuwa ni adhabu kali tu, zinazoweza kuwakomesha matapeli.

Wakati huo huo kashfa ya dawa ya Dioxin imevuka mipaka ya Ujerumani na kuingia katika nchi jirani.

Kampuni moja ya Uholanzi imeuziwa mayai 136,000 kutoka Ujerumani. Inahofiwa mayai hao yana sumu iliyogunduliwa nchini Ujerumani mapema wiki iliyopita.

Waziri wa kilimo wa Ujerumani Ilse Aigner pia amesema anataka pawepo uwazi juu ya mayai yaliyobakia.

Chanzo:DW-BONN

Waziri huyo alikuwa anajibu madai ya kampuni za uzalishaji wa chakula cha mifugo kwamba huenda dawa ya Dioxin iliingia kwa bahati mbaya katika chakula cha kuku.

Wakati huo huo idara kuu ya sheria ya Ujerumani imeanza kuzichunguza kampuni mbili zinazozalisha dawa za chakula cha kuku.

Wataalamu wamesema dawa ya Dioxin inayotokana na mabaki ya dizeli inaweza kusababisha maradhi ya saratani -yaani kansa.

Chama cha wakulima nchini Ujerumani kinadai fidia kutokana na hasara iliyosababishwa na dawa ya Dioxin.

Kamishna wa sera za afya wa Umoja wa Ulaya, John Dalli, ameitaka Ujerumani itoe taarifa iwapo mayai na nyama ya kuku yenye sumu imeingia katika nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.

No comments: