June 25, 2011

Waziri wa zamani Rwanda afungwa maisha

Mwanamke wa kwanza kushtakiwa kwenye mahakama ya kimataifa kufuatia mauaji ya kimbari nchini Rwanda amehukumiwa kifungo cha maisha jela.

Waziri huyo wa zamani wa masuala ya Familia, Pauline Nyiramasuhuko, amepatikana na hatia ya kupanga mauaji hayo na kuratibu ubakaji wa wanawake na wasichana wakati wa mauaji yaliotokea mwaka 1994.

Bi Nyiramasuhuko mwenye umri wa miaka 65, alifika katika mahakama ya uhalifu wa kivita nchini Rwanda (ICTR), ilioko mjini Arusha Tanzania leo.

Waziri huyo wa zamani na mtoto wake wa kiume Arsene Shalom Ntahobali, walikuwa wanakabiliwa na mashtaka kumi na moja, yakiwemo mauaji, ubakaji na kuwatesa watutsi na wahutu wenye msimamo wa wastani.

Mashtaka ya dhidi yake kuhusu ubakaji yalikubalika kwa kuwa korti iliridhika kuwa alijua wasaidizi wake walikuwa wanafanya vitendo hivyo lakini hakuchukua hatua kuwazuia.

Mahakama hiyo imeambiwa kuwa waziri huyo wa zamani na familia yake alishiriki kuunda vikundi vya wanamgambo waliotekeleza mauaji hayo.

Mahakama hiyo ilielezewa kuwa alihusika na mauaji yaliotokea maeneo ya kusini mwa jimbo la Butare.

Mahakama ya ICTR ilibuniwa mwaka wa 1994 kufuatia mauaji hayo ya kimbari ambapo inakadiriwa kuwa watu 800,000 waliuawa.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22