February 10, 2012

Bunge la Ujerumani kupiga kura kuhusu mpango wa kuiokoa Ugiriki

Wabunge wa Ujerumani watapiga kura mwishoni mwa mwezi huu kuhusu mpango mpya wa mabilioni ya euro wa kuuokoa uchumi wa Ugiriki. Volker Kauder, Mkuu wa kundi la wabunge wa chama cha Kansela Angela Merkel, Christian Democrats, amesema bunge litapiga kura Jumatatu tarehe 27 mwezi huu wa Februari kuhusu mwelekeo wa Ugiriki. Amesema lengo lao linasalia kuisaidia Ugiriki, lakini Ugiriki pia ni sharti itimize ahadi zake. Bibi Merkel alikutana na viongozi wa makundi yote ya bunge mapema leo, ili kuwaeleza kuhusu juhudi za kukubali kitita cha pili cha mkopo wa kuiokoa Ugiriki isifilisike, ijapokuwa mkataba thabiti bado haujaafikiwa. Mawaziri wa kanda ya sarafu ya euro, ambao hawajaridhika na mpango huo wa kubana matumizi, wameipa Ugiriki hadi Jumatano kutimiza masharti mengine ya mpango huo, ili wapokee mkopo wa euro bilioni 130. Merkel alishinda kura mbili muhimu bungeni kuhusu mzozo wa deni la kanda ya sarafu ya euro mwaka jana.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22