April 14, 2012

MSANII ALI KIBA ADAIWA KUHOJIWA NA POLISI KUHUSIANA NA MADAI KUWA NDO ALIMPATIA ELIZABETH MICHAEL 'LULU' LIFTI SIKU KANUMBA ALIYO FARIKI...!!!


Habari kutoka Mwanaspoti zinasema msanii wa muziki wa Bongo Flava, Ali Kiba, anadaiwa kuhojiwa na polisi kwa maelezo ndiye aliyempa Elizabeth Michael Lulu msaada wa usafiri (lifti) baada ya kutoka kwa Steven Kanumba.
Lulu ndiye anayetuhumiwa kuhusika na kifo cha Kanumba kilichotokea usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.


Kachero aliyemhoji Lulu Jumatatu wiki hii, amedai kuwa msanii huyo alihojiwa katika kituo cha Polisi cha Oysterbay kutokana na kutajwa na mtuhumiwa kuwa ndiye aliyempatia lifti baada ya kutoka kwa Kanumba.
Mwanaspoti lilimtafuta Ali Kiba ili azungumzie taarifa hizo, alipopatikana kwa njia ya simu, msanii huyo alisema: "Samahani kaka siwezi kuzungumzia chochote kuhusu mambo hayo."Kisha akakata simu.


Lulu alitoa maelezo yake polisi Jumatatu ikiwa ni saa 65 tangu kutokea kwa kifo cha Kanumba., ambapo alizungumza na kachero wa Makao Makuu ya Polisi ambaye pia ana taaluma ya saikolojia.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kachero huyo (jina tunalo) aliyetoka makao makuu alifanikiwa kufanya mahojiano na binti huyo ambaye awali aligoma. Imeelezwa kuwa, alitumia takribani sasa tatu kumlainisha Lulu azungumze.

Katika mahojiano na gazeti la The Citizen Jumanne, kachero huyo ambaye alitoka katika Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai alisema tayari amemhoji mtuhumiwa namba moja Lulu pamoja na msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya kufuatia kifo cha Kanumba, aliyefariki usiku wa kuamkia Jumamosi.

Akimnukuu Lulu katika mazungumzo yake, kachero huyo alisema Lulu aliitwa na marehemu Kanumba ili waweze kutoka (out) kwenda kwenye bendi ya Mashujaa ambayo ilikuwa inapiga kwenye kiwanja chao cha nyumbani, Vingunguti. Mtuhumiwa alionekana kutokuwa tayari, lakini marehemu akamlazimisha Kachero huyo alisema: Lulu anadai alifika nyumbani kwa marehemu saa tano usiku, lakini akiwa ameweka msimamo wa kutokwenda sehemu yoyote usiku ule, lakini Kanumba alikuwa akilazimisha ndipo yakatokea mabishano na marehemu akafunga mlango kwa funguo.

"Hata hivyo, baada ya ugomvi wa kama nusu saa hivi, Lulu alifanikiwa kuondoka chumbani humo na alifungua mlango kwa taharuki na kuondoka bila kujua kilichotokea nyuma, huku akimweleza ndugu wa marehemu kwamba Kanumba ameanguka."
Mpashaji habari wetu huyo alisema, kumekuwa na jumbe fupi za maneno kutoka kwa wanasiasa ambazo zimekuwa zinaingia kwenye simu ya kiganjani ya Lulu, zikiahidi kumsaidia.
Alionya kuwa kama wanasiasa wataanza kuingilia uchunguzi wa Polisi katika kesi hiyo ambayo imevuta hisia za watu wengi, wanaweza kuharibu mambo. Lakini yeye mwenyewe akionyesha kwamba yuko imara na anafahamu anachokifanya.

Kuhusu msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ali Kiba, kachero huyo alisema kwamba alihojiwa kutokana na kutajwa na mtuhumiwa kama mtu aliyempatia msaada wa usafiri (lifti) baada ya kutoka kwa Kanumba.

Kachero huyo alisema kutokana na taarifa ambazo wanaendelea kuzipata, kuna uwezekano watu wengi zaidi wakahojiwa ili kujiridhisha kabla ya watuhumiwa kuanza kupandishwa kizimbani baada ya upelelezi kukamilika.
Lulu alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jumatano wiki hii na kutotakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji.

No comments: