March 30, 2015

Uchaguzi Nigeria; wananchi watakiwa kuwa watulivu

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameipongeza Nigeria kwa kuendesha uchaguzi kwa kiasi kikubwa kwa amani na utaratibu mzuri.
Lakini Ban amewataka wananchi kuendeleza hali ya amani na kuwa na subira, na ameshutumu mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Waislamu la Boko Haram pamoja na makundi mengine ya wanamgambo waliojaribu kuchafua uchaguzi huo wa rais na bunge. Zoezi la kuhesabu kura linaanza rasmi mchana huu, na matokeo yanatarajiwa baadaye leo Jumatatu.
Muda wa kupiga kura waongezwa
Upigaji kura ulilazimika kufanyika kwa siku mbili bila kutarajiwa na baadhi ya majimbo ya kupigia kura yalifanya hivyo jana Jumapili baada ya matatizo kutokea katika matumizi ya teknolojia mpya yenye utata ya kuwatambua wapiga kura na mara nyingine hata wasimamizi wa vituo vya kupigia kura hawakufika mahali wanapotakiwa kusimamia kama mkaazi huyu alivyolalamika.
"Lalamiko langu ni kwamba tuko hapa tangu Jumamosi. Hatujamuona afisa wa tume jana,maafisa wengine hawakuja na hatuelewi kuna nini. Tunasubiri. Watu wako hapa tangu tulipotarajia kupiga kura, watu wamejitokeza tangu alfajiri".
Lakini mkuu wa tume ya taifa ya uchaguzi Attahiru Jega amesema tume yake ina imani kwamba lengo lake la kufanya uchaguzi ambao ni huru, wa haki , wenye kuaminika na wa amani linaelekea kutimia. Afisa wa tume hiyo Amina Zakari anathibitisha hilo.
"Hali iliyopo sasa ni kwamba uchaguzi ulifanyika kwa mafanikio katika maeneo mengi, lakini huwezi kutarajia uwe bila matatizo katika maeneo yote".
Matatizo ya kiufundi
Matatizo ya kiufundi katika zoezi la kupiga kura , hata hivyo , yalianzisha hamasa zinazoelekeza kuwa na uwezekano wa mzozo wakati chama cha rais Goodluck Jonathan cha PDP kupinga matumizi ya chombo hicho cha kutambua wapiga kura , kikisema vifaa hivyo havikufanyiwa majaribio ya kutosha.
Chama cha Buhari cha All Progressives Congress APC kinaunga mkono mfumo huo mpya kama seemu ya kuzuwia udanganyifu katika upigaji kura ambao umechafua chaguzi zilizopita.
Kundi la asasi za kijamii nchini Nigeria linaloangalia uchaguzi huo limeonya leo Jumatatu kuhusu udanganyifu katika uchaguzi huo , likisema linawasi wasi mkubwa kutokana na ripoti za majaribio katika majimbo kadhaa nchini humo kuvuruga zoezi la ukusanyaji wa matokeo jumla ya uchaguzi huo.

Chanzo. DW.


No comments: