April 24, 2008

KILA MTU ATAJUTA

Asalaam Aleykuom

Kulikuwa na kundi la watu likisafiri pamoja. Wakafika pahali penye ardhi ya mawe na ilikuwa usiku wa kiza kinene. Ghafla wakasikia sauti kali isiyojulikana itokapo ikiwaeleza kwamba atakayeokota mawe kwa usiku ule atajuta; vilevile na asiyeokota pia atajuta. Watu wote wakahamanika na kuchanganyikiwa. Itakuwaje hivi? Uokote au usiokote mawe utajuta tu ??!!! Kwa hiyo, baadhi yao waliokota mawe hayo, na wengine hawakufanya hivyo. Walipoamka asubuhi baada ya kufikamakwao; wakaona yale mawe yamegeuka na kuwa almasi. Wale wasiookota mawe yale wakaanza kujuta, 'Yalaiti ningeokota na mie pia.' Na wale waliookota pia nao walijuta, 'Yalaiti ningeokota mengi zaidi.' Ndugu yangu Mwislamu, huu ni mfano tu; lakini mfano huu ndivyo hivyo itakavyokuwa siku yako ya kuondoka duniani kwenye maisha ya muda tu na kuelekea Akhera kwenye maisha ya milele kwa namna vile Hadith ya Mtume wetu (S.A.W.) inayotuelezea kwamba kila mtu atajuta wakati pale anapokata roho. Akiwa ni mwovu basi atajuta kwa maovu aliyoyafanya na atatamani arudi tena duniani ili afanye mema apate kuepukana na adhabu inayomkabilimbele yake ambayo wakati ule ndio inajidhihirisha wazi mbele yake (kwani mtu anapotolewa roho yake basi Mola humwonyesha wapi mafikio yake kabla ya kufikishwa huko, hapo haihitajiki tena imani yako ya kuamini kama kuna adhabu). Na kama akiwa ni mwema basi pia atajuta kwa nini hakuzidisha mema yake akapata daraja ya juu zaidi ya ile anayoonyesha pale. Ndugu yangu Mwislamu, nakuusia pamoja na kuiusia nafsi yangu,tumche Mwenyezi Mungu (S.W.). Tuutumie muda wetu katika mambo ya kheri yatakayotusaidia huko tuendako kwenye maisha ya milele. Hebu kaa kitako ufikiri, ni masaa mangapi kwa siku unayatumia katika kufanya mambo ya kheri na masaa mangapi unayatupa bure kwa mambo maovu au hata ya upuuzi na wala hayatokusaidia chochote akhera. Je katika siku kamili; ni kiasi gani umekumbuka Mola wako kwa kusoma kitabu chake kitukufu na kumtaja? Na mara ngapi umemwomba msamaha (maghfira) kwa maovu unayoyatenda kila kukicha? Na mara ngapi umemtakia Rehma kipenzi chake Mtume wetu mtukufu(S.A.W.)? Ndugu yangu Mwislam, ni sababu gani inayotufanya tusimwabudu Mola wetu na wakati mtu hujijui na wala huna hakika kabisa ni wakati gani kifo kitakubishia hodi?Kifo kifo kipo nyuma yako, kwani kinapowadia huna pa kukimbilia. Kila unavyopitisha siku uelewe wazi kuwa ndivyo unavyopiga hatua mbele na kukaribia kifo chako. Hujijui kamwe ni miaka mingapi au ni siku ngapi au hata ni dakika ngapi zimebaki za wewe kuishi duniani. Kwa hiyo tujitahidi sana kujiandaa na safari hii ya ghafla isiyo na miadi wala wakati maalum kwa kufuata amri za Allah (S.W.). Ndugu yangu Mwislamu, saa hii tuliyonayo hapa, basi jua kwamba katika saa hii hii kuna wenzetu wanaumwa mahututi hata kaulihawana; kuna wenzetu wanaiaga hii dunia; kuna wenzetu wanafukiwa na udongo. Tumshukuru Mola wetu mimi nawe tu wazima tunavuta pumzi, basi kwa nini tuupoteze wakati huu? Tujitahidini sana kufanya ibada, tuzilainishe nyoyo yetu kwa kumtaja Allah na Mtume Muhammad (S.a.w), tuhifadhi Qur'ani katika nyoyo zetu kwani kila unapoihifadhi kifuani kwako ndio kadiri itakavyozidi kukuombea mbele ya Mola siku ya kiyama. Ndugu yangu Mwislam, kwa ushahidi wa Hadith za Mtume (S.A.W.), huko tendako si pa kufanya dharau kabisa. Kunaadhabu za pale unapotolewa roho ambazo ni kwa kadiri ya matendo yako mbali na uchungu wa roho yenyewe pale inapotolewa uchungu ambao hata Mtume wetu (S.A.W.) ambae ni kiumbe bora duniani na kipenzi cha Mola (S.W.) ameupata pia. Pia kuna adhabu za kaburi ambazo pia ni kwa kadiri ya matendo yako, mojawapo ni kubanwa na kaburi hadi mbavu zinapishana. Vilevile kuna adhabu ya siku ya mwisho, siku ya malipo, siku itakayopimwa mizani yako kwa yote uliyoyafanya na utavuna kile ulichokipanda katika dunia hii , siku ambayo utakayosimama mbele ya Mola wako na mbele ya umati na kusoma kitabu cha amali zako bila kuficha kitu, kwani hutoweza kuongopa wala kuficha chochote. Na adhabu ya siku hii ya mwisho huanza tu baada ya kufufuliwa hadi paletutakaposimama mbele ya Mola kuhesabiwa, na adhabu hii ni kubwa sana kiasi ambacho mtu ataomba arudi kaburini kuliko kukumbana na adhabu ya siku ya mwisho. Pia adhabu hii ni kwa kadiri ya matendo ya mtu, kuna waja wema Mola atawanusuru na adhabu hii. Adhabu itadumu mpaka itafikia kuanzia watu wa umati zote zilizopita hadi umati wetu watafikia kumwomba kiumbe bora wa viumbe wote na mpenzi wa Mola Muumba naye ni Mtume wetu (S.A.W.) akawaombee kwa Allah (S.W) ili watu wahesabiwe na wajijue wanakwenda wapi; kama ni peponi basi na aende na kama ni motoni pia bora aende kuliko adhabu ya hapo uwanjani pamoja na kuwa hata huo motowenyewe haujui ukali wake hata chembe. Ninachokuomba ndugu yangu Mwislam, tujihesabu kabla ya kuhesabiwa kama Mtume alivyotuusia. Kaa ujihesabu ni yepi mema uliyoyatekeleza na mangapi maovu uliyoyafanya katika kila siku yako moja unayoishi. Tunamuomba Mola Sub-haanahu Wataalaa atuepushe na adhabu zake, na atusameh madhambi yetu, na atanusuru na moto wake, na atujaaalie tuipate pepo yake kwa Rehma zake Inshaallah.
AMIN YA RABBIL-ALAMIM.

1 comment:

Anonymous said...

kAKA MALUMBO NIMEONA NA KUSOMA MSGE YAKO KATIKA BLOG YAKO, SAFI SANA NAMI NITAKUWA NASOMA MARA KWA MARA, NAWE USIACHE KUTUWAIDH, JE UNAKUMBUKA TULIKUWA TUNASWALI PAMOJA MSIKITI WA MTAMBANI WAKATI WA SHEKH ABUBAKAR KAULI? MIMI SINTO SAHAU WAKATI ULE.

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22