April 18, 2008

Mshike Mshike Berlin Kesho


Bayern Munich kesho jumamosi inapambana na Borussia Dortmund katika finali ya kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani.
Klabu ya zamani ya Pele-Santos imekata tiketi yake ya duru ijayo ya timu 16 za mwisho katika kombe la klabu bingwa za Amerika kusini-Libertadores cup.
Bayern Munich imeshatia mfukoni ubingwa wa Ujerumani ikiongoza kwa kileleni kwa pointi 10 na kesho ina miadi na Borussia Dortmund kwa finali ya kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) katika Uwanja wa olimpik wa Berlin .Ishara zote zaonesha Munich itatoroka na vikombe vyote 2 vya nyumbani msimu huu na hata kombe la Ulaya la UEFA.
Katika uwanja wa olimpik wa Berlin kesho, Borussia Dortmund itahitaji uchawi wake wote wa dimba kuutumia kuzuwia kaburi waliochimbiwa na Bayern munich jumapili iliopita walipochapwa mabao 5:0,lisiwazike tena kesho.
Bayern munich ikiwa imeshalitia kikapuni mwake taji la Bundesliga baada ya kufungua mwanya wa pointi 10,hawatazamii ubishi wowote kutoka Dortmund.
Ushindi wa mabao 5-0 ulifuatiwa na mwengine wa mabao 3-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt juzi jumatano.Mshambulizi wao wa kitaliana Luca Toni,amekuwa akiunasa wavu kila mechi na sielewi jinsi gani Dortmund watamzuwia kesho asitie bao jengine.
Kocha wa Dortmund Tomas Doll ana msukosuko mwengine,kwani masaa 48 kabla finali hiyo ya kesho,hakujua nani atalinda lango la timu yake.Kipa wao wa kawaida Weidefeller hataweza kucheza tena msimu huu na msaidizi wake hakuweza kucheza juzi kwavile ameumia goti.Kwahivyo, kocha Doll amesangaza kila mmoja alipoamua kumchagua kipa wa akiba wa safu ya 4 kujaza pengo hilo hapo kesho.Kwa kweli, kesho,Dortmund ili kuzuwia mvua ya magoli walionyeshewa jumapili iliopita isinyeshe tena, wangehitaji kipa nambari 1 kuzuwia dharuba ya akina Luca Toni, Miroslav Klose na hata Lukas Podolski.
Finali ya kesho itakua ya kipekee kwa kocha wa Bayern Munich,Ottmar Hitzfeld.Kwani ni yeye alieiongoza Dortmund kuutwaa kombe la klabu bingwa barani Ulaya 1997 kabla hakutorokea bayern Munich kuwa kocha wa huko.Hitzfeld akanyakua kombe hili la ujerumani miaka 2 mfululizo akiongoza Bayern Munich 2002 na 2003.
Wakati mashabiki wa Ujerumani wanpania kwa finali ya kombe lao la shirikisho la dimba, mashabiki wa Amerika kusini wanachangamshwa na Libertadores Cup-kombe la klabu bingwa za Amerika kusini:
Santos-klabu ya zamani ya Pele imetimua nje Cucuta kwa mabao 2-1 na imekata tiketi ya duru ijayo ya kundi la timu 16.San Lorenzo ya Argentina pia imeingia duru hiyo baada ya kuizaba Caracas Fc -mabingwa wa Venezuela mabao 3-0.
Santos kwahivyo imemaliza wapili katika kundi la 6 ikiwa na jumla ya pointi 10-moja zaidi kuliko Guadalajara ambayo ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa wa Bolivia,San Jose ulikuwa wa bure tu.
Caracas na San lorenzo zilianza mpambano wao wa kundi la kwanza mjini Buenos Aires wakiwa na pointi 7 kila mmoja huku wakiania nafasi ya pili nyuma ya Cruzeiro ambayo imeshafaulu kuingia duru ijayo.Caracas ikihitaji sare,lakini ilikua San lorenzo ndio iliotangulia mnamo dakika ya 16 na Rosales akaufumania mlango wake mwenyewe kwa bao jengine.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22