April 17, 2008

Ufisadi wa Fedha za Umma

Waziri wa Miundombinu Mh.Andrew Chenge akihojiwa na mapaparazi baada ya kutua Dar jana.

Waziri wa Miundombinu anayetuhumiwa kujilimbikizia mabilioni ya fedha nje ya nchi, Bw. Andrew Change, amerejea nchini na kukiri kuwa tuhuma zinazomkabili ni nzito na kwamba yuko tayari kufanyiwa uchunguzi. Hata hivyo, Bw. Chenge ametumia msemo wa `mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni`, bila kufafanua maana ya kuamua kutumia usemi huo. Hata hivyo, aliyaita mabilioni anayotuhumiwa kujilimbikizia kuwa ni vijisenti tu. Alidai kuwa tuhuma zinazomkabili huenda inawezekana ni za kuumba. Aidha, Bw. Chenge alisema, anawasiliana na mwanasheria wake ili kuona hatua za kuchukua dhidi ya vyombo vya habari vilivyoandika tuhuma hizo na kuvuka mipaka ya maadili ya uandishi wa habari. Hata hivyo, hakutaja hatua atakazochukua wala ni vyombo vya habari gani vilivyoandika na kuvuka mipaka ya maadili. Bw. Chenge aliwasili jana katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere akitokea nchini China alikokwenda kikazi na Rais Jakaya Kikwete. Tofauti na anavyokuwa siku zote jana wakati akiongea na waandishi wa habari Bw. Chenge alionekana mnyonge kidogo na akiwa katika hali ya tahadhari kubwa na mwangalifu kwa kila swali aliloulizwa. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa vyombo mbalimbali vya serikali na vya nje ya nchi vinavyomchunguza atavipa ushirikiano ili mwisho wa siku ukweli uweze kupatikana. Alipoulizwa kuwa tuhuma hizo zinaichafua kwa kiasi gani serikali ya Bw. Kikwete alisema, Watanzania wasubiri uchunguzi kwa madai kuwa na yeye ana historia kubwa katika nchi hii. ``Jamani na mimi nina historia kubwa katika nchi hii hivyo nipeni muda nitafakari tuhuma hizi,`` alisema. Alipoulizwa kama ni kweli amejilimbikizia mabilioni hayo ya fedha, Bw. Chenge hakusema ndiyo au hapana bali alidai kuwa watu wasubiri uchunguzi utakapokamilika. Na alipoulizwa kama atajiuzulu wadhifa wa uaziri aliendelea kujibu kwamba kwanza tuache uchunguzi ufanyike. Bw. Chenge alitokea mlango wanaotokea viongozi maarufu (V.I.P) akiwa amevaa suti na kuwafuata moja kwa moja waandishi ili wamuulize walichotaka kumuuliza. Baada ya kumaliza kujibu maswali yao yaliyochukua takribani dakika 10, huku baadhi ya wananchi wakiwa wamejazana nje ya geti, aliondoka na kurudi tena katika chumba cha (V.I.P). Jumamosi Aprili 12, gazeti la The Guardian la Uingereza liliripoti kwamba Bw. Chenge alikutwa akiwa na zaidi dola za Marekani milioni moja (sawa na zaidi ya sh. bilioni moja) katika akaunti yake iliyoko katika kisiwa cha Jersey nchini Uingereza. Wachunguzi wa Uingereza wanahisi kuwa pesa hizo ni mgao wa rushwa aliyopata ili kuipitisha Tanzania kununua rada ambayo imekuwa ikilalamikiwa sana kwamba gharama yake ilikuwa kubwa kuliko mahitaji, tena katika nchi maskini kama yetu. Wakati rada hiyo inanunuliwa, Bw. Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Uchunguzi kuhusu kama kuna rushwa katika sakata hilo la rada unafanywa na taasisi ya Uingereza ya SFO ambayo imekuwa ikihisi kwamba dola milioni 12 zilitolewa kama rushwa ili kuidhinisha ununuzi wa rada hiyo wakati wa utawala wa awamu ya tatu. Hata hivyo, kwa mujibu wa The Guardian, Bw. Chenge ambaye anatetewa katika sakata hilo na wakili wa Kimarekani, alikiri kwamba pesa hizo ni zake lakini akasema si rushwa na wala hazihusiani na sakata la rada.

1 comment:

Anonymous said...

tutafika tuu. huo ndio mwendo wetu. lazima matumbo ya wachache yashibe then matumbo ya wengi (masikini). kwa bahati mmbaya matumbo ya matajiri au mafisadi huwa hayashibi. sijui itakuwaje katika kujenga nchi yetu na wengi wenye njaa!!

heri

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22