Kabla ya mchezo huo, mengi yalitarajiwa, mengi yalihofiwa na tetesi nyingi zilisikika. Suali lililokuwa linaulizwa: Jee mchezo huo utaupiga jeki ule mwito wa kutaka kuweko maingiliano baina ya Wajerumani na Waturuki hapa nchini? Jee kutatokea fujo katika maeneo yalio na matatizo ya Kreuzberg na Neukölln huko Berlin? Na jee uhusiano baina ya Ujerumani na Uturuki utabadilika? Kandanda sio siasa, lakini ni tu kitu kilicho kizuri pembezoni mwa maisha yetu hapa duniani.
Ujerumani sasa itaingia finali ya kuwania Kombe la Kabumbu la Ulaya hapo jumapili ijayo mjini Vienna. Ni heshima. Waturuki jana walionesha mchezo mzuri, lakini kwa bahati mbaya walishindwa. Hata hivyo, waliondoka uwanjani mabega juu, na jambo hilo pia lilikuwa zuri. Mwishowe bahati ndio ilioichora bendera ya Ujerumani ya rangi nyeusi, nyekundu na ya dhahabu.
Ukiondoa visa vidogo vya hapa na pale, ile michafuko iliohofiwa itatokea haijaonekana. Waturuki walisherehekea kwa wingi katika miji ya Ujerumani bega kwa bega na Wajerumani. Na baada ya mchezo walipongezana,Wajerumani wakirandaranda mabarabarani katikati ya miji, magari yao yakipiga honi kwa nguvu. Waturuki walipigia tu makofi jambo hilo na wao pia kupiga honi za magari yao. Sasa nao Waturuki wanaweza kuiunga mkono Ujerumani katika pambano la finali. Wanafanya hivyo kila wakati,isipokuwa tu pale inapohusika Uturuki.
Baada ya miito iliotolewa kiwanjani kabla ya mchezo na manahodha wa timu hizo mbili, Michael Ballack wa Ujerumani na Rüstü Rencber wa Uturuki, wakipinga ubaguzi wa rangi, ilikuwa muhimu kwamba timu zote mbili zicheze kwa nidhamu. Hakujakuweko fauli mbaya, maamuzi ya mabishano na ugomvi baina ya wachezaji. Ule uungwana na urafiki baina ya wachezaji uliokuweko kiwanjani ulisambaa pia nje ya mji wa Basel, hata katika miji ya hapa Ujerumani. Hali kama hiyo ilishuhudiwa huko Uturuki.
Kabla ya mchezo huo kulizungumziwa juu ya sherehe ya kuendeleza maingiliano baina ya Wajerumani na Waturuki. Sasa picha za jana zimesababisha hisia kwamba matarajio hayo yanaweza kutimia. Lakini itakuwa pia kutia chumvi tukitarajia kwamba kandanda tu litafuta makosa yanayofanywa na serekali, wanasiasa na vyama vyao katika masuala ya maingiliano baina ya watu na kuweko hali ya kustahamiliana ndani ya jamii. Mchezo wa kandanda hauna uwezo huo, na utakuwa umeelemewa sana pindi tukiubebesha mzigo huo.
Kwamba mchezo huo mzuri wa jana sasa utatoa motisha mpya, kama vile watu wangependa kufikiria, haitarajiwi. Maisha ya kila siku ya Waturuki na Wajerumani yamejengeka na ati ati na, kwa upande mwengine, matarajio makubwa. Mchezo wa kandanda unabaki kuwa ni kitu kizuri pembeni mwa maisha yetu hapa duniani, pia kwa Wajerumani na Waturuki. Hata hivyo, wasiwasi unabakia. Waturuki wanahisi hawafahamiki vizuri kwa Wajerumani wengi, na Wajerumani nao hawaiamini ile nia ya Waturuki ya kutaka kujichanganyisha katika jamii ya Ujerumani. Hofu ya Wajerumani kuelekea utamaduni na dini nyingine ya Waturuki, kwa bahati mbaya, itaendelea kuweko, na jambo hilo halitabadilishwa na kandanda.
Wahnsinn! Unsere Nerven!
No comments:
Post a Comment