Mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha sheria mpya kuhusu uhamiaji sheria ambazo zinakosolewa mno na baadhi ya mataifa ya Afrika na Amerika ya Kusini.Hata hivyo katika kikao cha mjini Brussels Ubelgiji hii leo mawaziri hao wameshindwa kufikia uamuzi wa pamoja kuhusiana na mpango maalum unaojulikana kama Blue Card ambao unalenga kutoa nafasi kwa wageni walio na ujuzi wa kikazi kuja kufanya kazi barani Ulaya.
Katika mkutano huo wa Brussels mawaziri wa mambo ya nje wamesaini mpango unaozihusu nchi zote za Umoja wa ulaya juu ya masuala ya uhamiaji na uombaji hifadhi ya ukimbizi hatua ambayo sasa imefungua njia kwa viongozi wa Umoja huo wa ulaya kuudhinisha mpango huo ambao unakosolewa vikali na baadhi ya nchi za Afrika na Amerika ya Kusini.
Kwa mujibu wa mpango huo nchi zote za Umoja huo wa Ulaya zitashirikiana katika kukabiliana na suala zima la uhamiaji na uhamiaji haramu kwa kushirikiana na nchi ambazo wanatokea wahamiaji au nchi ambazo wahamiaji wanapitia kuingia barani ulaya.
Mpango huo pia unataka paweko njia madhubuti za kudhibiti mipaka wakati sera bora ya uhamiaji ikiandaliwa.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Wolfgang Schauble akizungumza katika kikao hicho amesema kwamba mpango huo ni hatua muhimu ya kusonga mbele akiongeza kwamba.
Makubaliano hayo yanafungua njia ya kuwepo uhamiaji halali kwa watu wenye ujuzi wa kazi mbali mbali au wataalamu ambao ujuzi wao unahitajika katika nchi hizo.Mawaziri hao pia wamekubaliana kujaribu kuzuia utoaji kwa wingi wa vibali vya kuishi katika nchi zao.Italy na Uhispania zimewakasirisha mawaziri wengine wa nchi za umoja huo kwa kutoa hati hizo kwa kiasi cha watu 700,000 katika miaka ya hivi karibuni.
Kutokana na mpango huo sasa itawabidi wakimbizi kulazimika kuomba hifadhi wakiwa nje ya nchi hizo.Kiasi cha watu 220,000 walifanya hivyo mwaka jana ingawa Umoja wa Ulaya umesema utaongeza misaada katika nchi ambazo watu wanazikimbia.
Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Liam Byrne akizungumza kwenye kikao hicho amesisitiza kwamba ni muhimu kuyatekeleza mawazo yaliyotolewa kivitendo ili kukabiliana na hali iliyoko sasa.
Aidha waziri huyo amesema wiki ijayo atakwenda nchini Ufaransa kwa lengo la kuzungumzia juu ya utekelezaji wa haraka wa njia za kukabiliana na wahamiaji na hasa kuhusu mpango wa pamoja wa kuwarudisha nyumbani wahamiaji haramu.
Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuudhinsha mpango huo katika mkutano wa kilele utakaofanyika Oktoba 15 na 16.
Kwa upande mwingine mawaziri hao hawajapata ufumbuzi juu ya suala la wafanyikazi wenye ujuzi wa hali ya juu ambapo baadhi wanakubali pendekezo kwamba watakaokubaliwa maombi yao watabidi kulipwa mshahara mara moja na nusu zaidi ya kiwango cha mshahara wa kawaida katika nchi watakakokubaliwa kufanya kazi.
Wafanyikazi hao pia itabidi wawe na ujuzi wa miaka mitano katika nchi zao.Katika nchi nyingi za ulaya kiwango cha idadi ya watu kimeanza kupungua na nchi hizo zinatafuta wafanyikazi kutoka nje ili kujaza nafasi za kazi fulani fulani lakini nchi hizo zinajaribu kushindana na Marekani ambayo inawavutia kiasi cha mara mbili ya idadi hiyo ya wafanyikazi wenye ujuzi.
Mpango wa Blue Card ambao jina lake limetokana na bendera ya Umoja wa Ulaya yenye rangi ya Buluu na nyota za rangi ya dhahabu na ambao jina lake linawiana na mpango wa Marekani wa Green Card,utatoa nafasi kwa wafanyikazi wenye ujuzi wa hali juu kutoka nchi zinazoendelea kupata haki mbali mbali katika nchi za Umoja huo wa Ulaya.
Wakati huohuo halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imekubali kuongeza msaada wa kiutu nchini Zimbabwe kwa euro millioni 10 fedha ambazo zitatumika katika masuala ya huduma za afya,maji na huduma nyingine za kibidamu.Lengo kubwa la kutolewa msaada huo ni kutatua matatizo ya idadi kubwa ya wazimbabwe wanaoteseka kufuatia ghasia.Msaada huo umetajwa kwamba hauhusiani na mpango wowote wa kisiasa nchini humo.
No comments:
Post a Comment