October 20, 2008

POWELL'AMFAGILIA' OBAMA

Mgombea urais wa Marekani kwa kutumia tiketi ya chama cha Democratic Barack Obama amepata msukumo katika kampeni yake kufuatia kuungwa mkono na waziri wa zamani wa mashauri ya kigeni wa nchi hiyo tena kutoka chama cha upinzani cha Republican Colin Powell.
Mtu mashuhuri nchini Marekani ambae anaheshimiwa na wanasiasa pamoja na wanajeshi, Generali Mstaafu Colin Powell ambae alivunja daftari za historia ya Marekani kwa kuwa mtu mwenye asili ya Kiafrika wa kwanza kutumika kama waziri wa mashauri ya kigeni wa nchi hiyo na pia kuwa mkuu wa majeshi amesema kuwa anamuunga mkono mgombeaji wa chama cha upinzani Barack Obama.
Hatua ya Colin Powell Generali Mstaafu imekuja kukiwa kumesalia wiki mbili kabla ya kufanyika kura Novemba 4.Hatua hiyo imeipiga jeki kampeni ya Obama, ambae tayari anaongoza mpinzani wake wa chama cha Republicans seneta John McCain katika kura za maoni. Kwa upande mwingine upande wa kampeni wa Seneta Obama unasema kuwa Obama amefanikiwa kukusanya pesa zaidi za kuendesha kampeni. Inasemekana mwezi Septemba kiliweza kukusanya dola millioni 150.
Hii imevunja rikodi yake ya mwezi Agosti ambapo aliweza kukusanya dola millioni 66.
Seneta Obama alipokuwa anahutubia wafuasi wake zaidi ya laki 10,amesema kuwa, amepokea kwa unyenyekevu uungwaji mkono wa Colin Powell na pia inasemekana alimpigia simu kumshukuru kwa hatua hiyo.
Yeye Seneta McCain, licha ya kuwa hatua ya Powell inaonekana kama ni pigo lakini yeye amesema kuwa hajashtushwa na hatua hiyo.
Powell ameongeza kusema kuwa anashindwa kuelewa hatua ya baadhi ya wanachama hicho cha Republicans,bila kumtaja McCain,ambao wanaendelea kusema ama kukubali wengine kusema kuwa Obama ni Muislamu huku ni mkristo. Akaongeza kuwa je kuna ubaya gani ikiwa ni muislamu?
Kuhusu McCain, Powell amesema kuwa amemkuta Seneta Mccain kama asie na uhakika jinsi ya kushughulikia masuala ya kuichumi walio nayo.
Powell ni mwanachama wa chama cha Republicans na alikuwa mwanadiplomasia namba moja wa rais George W.Bush na anabeba jukumu la mchango wake katika kuchochea uvamizi wa Iraq.Uungaji wake huu kwa seneta Obama ni pigo kubwa kwa McCain na unaweza kusaidia kushawishi kura za wanajeshi wa zamani pamoja na za wale ambao huwa baado kuamua wampigie nani kura.

No comments: