December 19, 2008

Ban apongeza hukumu dhidi ya Bagosora

Theoniste Bagosora 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki-Moon amepongeza hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Mauaji ya Rwanda (ICTR) ya mjini Arusha Tanzania, dhidi ya maafisa wa ngazi za juu wa Rwanda kwa kushiriki katika mauaji ya halaiki ya mwaka 1994.

Ban Ki-Moon amesema hukumu hiyo ya ICTR ni hatua muhimu dhidi ya hofu ya kuwaadhibu viongozi wanaohusika na makosa makubwa ambayo yanaangaliwa kimataifa.

Mahakama hiyo jana ilimhukumu mkurugenzi wa zamani wa wizara ya ulinzi ya Rwanda, Theoniste Bagosora kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kuhamasisha mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Bagosora, mwenye umri wa miaka 67 anaungana na maafisa wengine wa zamani wa jeshi la Rwanda, Kanali Anatole Nsengiyumva na Meja Aloys Ntabakuze, waliohukumiwa pia kifungo cha maisha jela kutokana na kuhusika na mauaji hayo yalisababisha vifo vya watu 800,000.

Wakati huo huo, muandaaji wa vijana walioshiriki katika mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994 aliyehukumiwa kwa ukiukaji wa ubinaadamu wakati wa mauaji hayo ameachiwa huru leo baada ya kutumikia kifungo cha miaka 7 jela. Akizungumza baada ya kuachiwa huru, Joseph Nzabirinda alisema anaandaa mipango ya kwenda kuungana na familia yake nchini Ubelgiji.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22