January 05, 2009

TAHADHARI KINA DADA WANAOPENDA LIFT

Ujambazi wa aina yake wa kutumia magari mazuri umeibuka jijini Dar es Salaam ambapo walengwa wakubwa wakiwa wanawake kwa kuibiwa vitu vya thamani na wengine kufanyiwa vitendo vya kinyama. 
Matukio hayo yanatokea katika maeneo mbalimbali jijini hapa na wanawake kadhaa wamejikuta wakiingia kwenye mitego hiyo bila kuwashtukia watu wanaofanya ujambazi huo. 
Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa matukio hayo na tayari watu watatu wameshatiwa mbaroni na kupelekwa mahakamani. 
Limetahadharisha watu kuwa makini na watu hao na mara wanapoona matukio hayo watoe ripoti mara moja polisi. 
Majambazi hao hutumia magari mazuri ya kifahari ili walengwa wasiwatilie mashaka wanapowanasa kwenye mitego yao. 
Katika tukio moja lililotokea maeneo ya Oysterbay karibu na kituo cha ubalozi wa Marekani wa zamani, msichana mmoja Mariamu Hussein, anayefanyakazi katika ofisi moja eneo hilo, alisema wakati akitoka ofisini kuelekea kituo cha basi, gari aina ya baloon lilisimama karibu yake na ndani ya gari hilo kulikuwa na kaka aliyemfahamu kwa sura kwa kuwa ni mteja katika ofisi yao. 
Alisema kaka huyo alimuuliza anakwenda wapi na kumwambia aingie kwenye gari ili amsogeze anakoelekea. 
Mariamu alisema aliingia kwenye gari na walipofika karibu na kilima cha mataa ya kuelekea njia panda ya kanisa Katoliki la St. Peter`s, dereva alianza kustua gari kama vile lilikuwa na tatizo. Alisema baada ya kujifanya kulistua kwa muda, aliliingiza gari hilo kwenye kituo cha mafuta karibu na mataa hayo na kumuomba ashuke ili amsaidie kusukuma. ``Wakati nateremka kwenye gari nilitaka kuchukua pochi langu, lakini yule dereva aliniambia niliache tu kwani tutasukuma kidogo tu na kuwaka,`` alisema Mariamu. 
Alisema aliliacha pochi lake na kuanza kusukuma gari hilo na lilipowaka, dereva aliwasha moto na kutokomea na gari huku pochi lake lililokuwa na vitu vya thamani, fedha na kadi za benki likiwa limeyeyuka. 
Katika tukio lingine mkazi wa Msasani ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema alikuwa ametoka Karikoo kununua mahitaji ya nyumbani pamoja na nguo na kuviweka kwenye mfuko mmoja. 
Alisema akiwa karibu kabisa na nyumbani kwake, alisimama na kusalimiana na rafiki yake na alipomaliza alianza kuelekea nyumbani kwake. 
Mkazi huyo alisema wakati anaongoza kwenda nyumbani, mbele yake aliona gari jeupe zuri ambalo lilikuwa na watu wawili (mmoja dereva na mwingine alikuwa ameketi kiti cha abiria). 
Alisema gari hilo lilikuwa linatembea taratibu na yule mtu aliyekuwa ameketi kiti cha abiria alitoa kichwa chake nje na kuanza kuangalia tairi la nyuma kitendo kilichoashiria kuwa huenda gari hilo lilikuwa na tatizo. 
Mkazi huyo aliendelea kusimulia kuwa gari hilo lilipomkaribia, yule abiria aliyejifanya kuangalia tairi, alimkwapua mfuko wake kitendo kilichofanyika kama umeme na gari liliondolewa kwa kasi ya ajabu. Aidha, katika tukio lililotokea maeneo ya Sinza Madukani, dada mmoja ambaye pia hakupenda jina lake litajwe gazetini, alisema alinusurika kufanyiwa kitu kibaya baada ya kuchukua taxi na kutaka apelekwe Tabata. Alisema walipofika eneo la Ubungo mataa, dereva huyo aliingiza gari kituo cha mafuta na kudai kuwa mafuta yamepungua. 
Hata hivyo, dada huyo alisema dereva huyo alichukua muda mrefu bila kurudi kwenye gari kitendo kilichomtia wasiwasi na kuamua kupiga simu kwa dereva taxi mwingine aliyezoea kumchukua. 
Alisema alipomwambia kuhusu taxi hiyo na kumtajia namba za gari, alimwambia ateremke haraka kwani huyo alikuwa `deiwaka` ambaye alikuwa akijihusisha na vitendo vya kijambazi vya kuteka wanawake na kuwaibia vitu vyao vya thamani na hatimaye kuwabaka. 
Akiongea na Nipashe Jumapili Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Evarist Mangala, alikiri kupokea taarifa za matukio hayo yakiwemo ya watu kupewa `lift` na kuambiwa wasukume magari. 
Hata hivyo, alisema hajawahi kupokea taarifa za wizi wa vifurushi kwa kutumia magari lakini polisi ilishatoa tahadhari kwa wananchi kuepuka kupanda `lift\' kwenye magari ya watu wasiowafahamu. 
`Inapotokea umepata `lift` ukaombwa usukume gari, chukua vitu vyako usiviache kwenye gari,`` alisema.

No comments: