January 22, 2009

UCHUMI WA UJERUMANI KUDONDOKA

Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Michael Glos, akiionesha hadharani ripoti juu ya makisio ya uchumi wa Ujerumani kwa mwaka 2009
Kwenda chini uchumi wa dunia kumeathiri pia uchumi wa Ujerumani
Yule ambaye ana hamu na masuala ya uchumi na siasa za fedha, basi hawezi kutoijali ripoti ya mwaka ya serekali ya Ujerumani kuhusu uchumi, na hasa katika wakati huu wa mzozo. Ripoti hiyo inatoa maelezo ya undani vipi serekali inavoitathmini hali ya mambo na vile inavoshughulikia kuona uchumi unapanda kwa njia ilio imara. Inahitaji kufanywa kazi nyingi. Hata hivyo, zaidi ya thuluthi mbili ya wananchi wa Ujerumani hawaamini kwamba Euro bilioni 50 zilizotolewa na serekali zinaweza kusaidia kuupiga jeki mpango wa kuunyanyua uchumi na kuiongoza nchi hii bila ya kupata mapigo kutokana na kwenda chini uchumi duniani kote.
Sasa ni rasmi kwamba Ujerumani iko katikati ya hali ya uchumi wake kwenda chini. Nikimnukuu waziri wa uchumi wa Ujerumani, Michael Glos, anasema:
" Kwa mwaka mzima wa 2009, tunatarajia uchumi kurudi nyuma kwa asilimia mbili na robo. Kwa kwenda huku chini uchumi, ambako, kwa bahati mbaya, lazima tuukadirie, hakuna mfano wa aina hiyo katika historia tangu kumalizika vita vikuu vya pili. Ni kwenda chini sana uchumi katika historia ya karibuni ya Ujerumani."
Asilimia hiyo mbili na robo ni kima cha mwaka.
Juzi, Tume ya Umoja wa Ulaya ilisema uchumi wa Ujerumani utanywea kwa asilimia 2.3 mwaka huu, na uchunguzi wa maoni ya wananchi uliofanywa na jarida la STERN linalochapishwa kila wiki hapa Ujerumani umeonesha kwamba Wajerumani wengi wanautilia ati ati mpango wa Kansela Angela Merkel wenye thamani ya Euro bilioni 50 ili kuupiga jeki uchumi, kama mpango huo utaweza kuulinda uchumi mkubwa kabisa wa hapa Ulaya na mporomoko wa uchumi unaoonekana sasa duniani. Ni asilimia 26 ya watu walioulizwa ambao walisema wana imani kwamba mpango huo wa Kansela Merkel, ambao ni pamoja na kutumia fedha kwa ajili ya miradi ya miundo mbinu na kutoa nafuu kwa wanunuzi wa magari mapya pamoja na kuwapunguzia watu kodi za mapato, utasaidia kuunyanyua uchumi wa nchi.
Uchunguzi huo wa maoni ya watu uligundua kwamba asilimia 56 waliikataa mipango ya serekali ya kulipa Euro 2,500 kwa kila mnunuzi wa gari ambaye ataiangamiza gari yake ya zamani na badala yake kununua gari mpya isioharibu mazingira, gari ambalo halitatoa moshi mwingi hewani. Watu hao waliokataa wanasema hatua hiyo sio nzuri katika kukabiliana na mzozo ulioko katika sekta ya biashara ya magari.
Robo tatu ya watu walioulizwa walisema hawana mipango ya kutumia nafasi hiyo ya nafuu iliotolewa na serekali, huku asilimia 11 tu wakisema watafikiria kuutumia motisha huo.
Kwa hivyo, leo serekali ya Ujerumani imesahihisha makisio yake ilioyatoa Oktoba mwaka jana kwa asilimia 0.2. Tangu wakati huo, tarakimu zinaonesha kumekuweko upungufu wa mauzo ya Ujerumani katika nchi za nje, jambo ambalo lilikuwa ni kama injini ya kukuwa uchumi wa Ujerumani katika miaka ya karibuni. Serekali inakadiria kwamba thamani ya bidhaa zake za kwenda ngambo itapungua kwa asilimia 8.9 mwaka huu. Mapato ya uchumi wa ndani wa Ujerumani yalikuwa mabaya sana mwaka 1975, pale uchumi ulipokwenda chini kwa asilimia 0.9.
Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Michael Glos, alisema nchi yake bado ni bingwa wa dunia katika kuuza bidhaa ngambo, bado Ujerumani ni nchi ya kibiashara nambari moja duniani. Nchi hii imefaidika na kwenda juu uchumi duniani, na bila ya shaka kinyume na hivyo hivi sasa, na hivyo ndivyo ilivyo sasa ambapo uchumi wa nchi hasa umeathirika. Wakati viwanda vya magari hapa nchini vimewapunguzia wafanya kazi wake masaa ya kufanya kazi, biashara ya ujenzi wa mashine, ambayo ndio bendera ya uchumi wa Ujerumani katika kusafirisha nje bidhaa, imebakia bila ya kuathirika. Kuangiziwa mashine za Ujerumani na wateja wa nchi za nje, bado kuko vile vile.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22