February 05, 2009

GADDAFI NA MUUNGANO WA AFRIKA


Mwenyekiti wa sasa wa Umoja  wa Afrika,Muammar Gaddafi wa Libya anaupa kipaumbele mradi wa kuundwa muungano  wa Afrika .Lakini wadadisi wa masuala  ya  kimataifa wanasema lengo hilo bado lipo mbali na hali halisi.

Gaddafi aliekuwa kiongozi  wa pekee kutoka  kaskazini mwa Afrika kuhudhuria mkutano wa viongozi  wa Afrika mjini Addis Ababa, alipokea kijiti kutoka kwa mwenyekiti wa hapo awali rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Kwa mujibu wa  taratibu za Umoja wa Afrika AU Gaddafi  atakuwa mwenyekiti wa Umoja  huo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Yumkini kipindi hicho kitakuwa fursa kwa Gaddafi kujaribu kuleta mapinduzi kwenye  Umoja wa  Afrika.

Wazo la Gaddafi linafahamika- anataka kuundwa kwa serikali moja kwa Afrika nzima, na anataka Afrika iwe na jeshi moja la askari  milioni 2. Kiongozi huyo wa Libya pia anataka Afrika iwe na sarafu, na pasipoti moja. Gaddafi amekuwa analea wazo hilo tokea mwaka 2007. Lakini wazo hilo lilipingwa na jirani zake.

Safari hii pia amekuja na pendekezo juu ya kuundwa Umoja wa Afrika-United States of  Afrika. Pendekezo hilo lilijadiliwa Addis   Ababa lakini halikuleta mabadiliko ya kina kirefu kwenye Umoja wa Afrika.

Hatahivyo nchi za Afrika zimekubaliana kuunda mamlaka mpya ya Umoja wa Afrika itakayochukua nafasi ya kamisheni ya hapo awali.Mamlaka hiyo inapaswa kuwa na jukumu kubwa zaidi,fedha zaidi na kuwa na uhuru   mkubwa katika kutekeleza wajibu wake. Gaddafi ametangaza kuwa,katika msingi wa mabadiliko hayo,  Muungano wa Afrika  utaundwa kwenye kikao kifuatacho cha nchi  za Umoja wa Afrika mnamo miezi sita ijayo!

Lakini aliekuwa mkurugenzi wa taasisi ya mjini Hamburg ya mitaala ya kimataifa ya Rolf Hofmeier amesema  kuwa lengo hilo bado lipo mbali. 

Mkurugenzi huyo pia ametabiri kuwa Umoja wa Afrika utakabiliwa na matukio ya ugeugeu  mnamo kipindi cha mwaka mmoja ujao  kutokana na uenyeketi wa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.

Hatahivyo mtaalamu wa siasa, Issa Shivji wa  Tanzania amesema wazo la kuundwa  muungano wa Afrika linastahili kuungwa   mkono.

No comments: