February 05, 2009

OBAMA NA UCHUMI WA AMERIKA


Baraza la senati nchini Marekani limepiga kura kurekebisha kipengele chenye utata katika mpango wa kuinua uchumi wa taifa hilo baada ya kutolewa onyo na nchi za Ulaya na Canada  kwamba kipengele hicho huenda kitazusha mvutano wa kibiashara na nchi zingine duniani. Kipengele hicho kinasisitiza zaidi kwamba watu wanunue bidhaa za Marekani. Kwa upande mwingine rais wa Marekani Barack Obama amezindua mipango ya kupunguza viwango vya mishahara ya wakurugenzi watendaji wa masoko ya hisa yanayotafuta usaidizi wa serikali. Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari rais Obama pia aliyakosoa makampuni ya fedha kwa kutowajibika wakati ambapo nchi hiyo inakabiliwa na mporomoko mkubwa wa kiuchumi. 

''Huu ni ukosefu mkubwa wa uwajibikaji, inatia aibu na vitendo hivi vya kupuuza gharama na athari zinazofuata ndio chanzo hasa kilichosababisha mgogoro huu''

Kanuni hizo mpya zitawapunguzia kiwango cha mishahara wakuu hao wa masoko ya hisa yanayopokea msaada wa kifedha kutoka kwa serikali na kufikia dolla laki tano kwa mwaka. Ripoti ya hivi karibuni inaonyesha kwamba makampuni hayo yaliwalipa wakuu hao zaidi ya dola billioni 18 kama malipo ya ziada mwaka jana. Wakati huo huo, rais Obama pia amesaini mswada unaopanua huduma ya bima ya afya kuwafikia watoto millioni 4 ambao walikuwa hawana bima hiyo akisema ni hatua muhimu katika kutimiza ahadi yake aliyotoa wakati wa kampeini ya uchaguzi kwamba atahakikisha kila mmoja anapata bima ya afya.

No comments:

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22