February 07, 2009

MKUTANO KUHUSU MAMBO YA USALAMA MUNICH

Frank-Walter Steinmeier

Mkutano muhimu wa kila mwaka juu ya usalama wa dunia umeanza leo mjini Munich ambapo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa wanashiriki. Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden pia anashiriki kwenye mkutano huo.

Viongozi wa nchi na serikali wanaohudhuria mkutano huo wa siku tatu uliofunguliwa na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier wanajadili masuala ya kupunguza silaha, mgogoro wa Mashariki ya Kati, hali ya nchini Afghanistan na mzozo wa nyuklia wa Iran.

Kufuatia kuingia madarakani kwa rais Barack Obama pana matumaini makubwa juu ya mkutano huo kuweza kumaliza zama za uhusiano wa mashaka mashaka baina ya Marekani na Urusi. Hatahivyo Urusi inawakilishwa na naibu waziri wa mambo ya nje kwenye mkutano huo Sergei Ivanov.

Kwa muda mrefu Marekani imekuwa inashiriki kwenye mikutano hiyo kwa kupeleka wajumbe wa ngazi za uwaziri lakini safari hii makamu wa rais wa nchi hiyo Joe Biden anashiriki mjini Munich.

Wachunguzi wa masuala ya kimataifa wanasema hiyo ni ishara ya dhamira ya utawala mpya wa Marekani juu ya kuleta mabadiliko katika sera zake za nje.

Bwana Biden, hapo baadae atawahutubia wajumbe zaidi ya mia tatu kutoka nchi zipatazo 50, wanaojadili masuala ya upunguzaji wa silaha za nyuklia,Iran na Korea ya kaskazini.

Katika hotuba yake bwana Biden anatarajiwa kufahamisha juu ya mtazamo mpya kuhusu mpango wa Marekani wa kuweka mtandao wa ulinzi wa makombora.

Utawala wa Marekani wa hapo awali ulikuwa unakusudia kutandaza mtandao huo barani Ulaya kwa kuhoji kwamba una lengo la kukabili hatari kutoka Iran.Lakini mpango huo umeikasirisha Urusi.

Mjumbe wa Iran Ali Larijani anaeuhudhuria mkutano wa mjini Munich atashiriki kwenye mjadala juu udhibiti wa silaha na hususan juu ya silaha za nyuklia.

Lakini ameazimia kutozungumzia mpango wa nyuklia wa nchi yake. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton ameashiria kuwa atatumia fursa zilizopo kushauriana na Urusi juu ya njia za kuzuia harakati za kinyuklia za Iran.

Katika siku ya mwisho ya mkutano huo jumapili,wajumbe watajadili hali ya Afghanistan ambapo majeshi ya kimataifa yanayoongozwa na Nato yanashiriki katika kulinda amani nchini humo.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan pia anahudhuria mkutano wa mjini Munich....

No comments: