February 27, 2009

MULUZI AKAMATWA KWA TUHUMA ZA UFISADI

Aliyekuwa rais wa Malawi Bakili Muluzi amekamatwa kwa tuhuma za wizi wa dola milioni 11 , pesa za msaada kwa nchi, kwa mujibu wa kitengo cha kitaifa cha kupambana na ufisadi.
Kitengo hicho cha kupambana na ufisadi kimesema Muluzi ameshtakiwa kwa makosa 87 kwa madai ya kuzielekeza kwa ujanja pesa za msaada katika akaunti yake binafsi.
Rais huyo wa zamani anatazamiwa kufikishwa mahakamani mjini Blantyre ambako mamia ya wafuasi wake wamekusanyika .
Muluzi, ambaye pia ni mgombea wa kiti cha urais kwenye uchaguzi wa mwezi Mei amekanusha kutenda kosa lolote, na amepinga uhalali wa uchunguzi uliofanywa na kitengo hicho cha kupambana na ufisadi.
Mwandishi wa BBC mjini Blantyre anasema rais huyo wa zamani alikamatwa baada ya kufika kwenye afisi za kitengo hicho cha kupamba ana na ufisadi siku ya Alhamisi, alipokwenda kujibu tuhuma dhidi yake.
Anasema maafisa wa Polisi wapatao 50 na wafuasi 1000 wa Bwana Muluzi wamekusanyika nje ya mahakama mjini Blantyre.
Wakili wa rais huyo wa zamani Jai Banda ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Muluzi alitumia haki yake ya kukataa kuzungumza alipoulizwa maswali na maafisa wa kitengo hicho.
Bwana Muluzi ambaye alitawala taifa hilo la kusini mwa Afrika kuanzia 1994 hadi 2004 , kwanza alikamatwa kuhusu tuhuma hizo mnamo mwaka 2006 lakini kiongozi wa mashtaka wakati huo akaitupilia mbali kesi hiyo.
Wafuasi wake wanasema kesi hiyo imechochewa kisiasa ili kumzuia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Uchunguzi huo unatokea huku kukiwa na wasi wasi wa kutokea ghasia kabla ya uchaguzi huo wa urais.
Rais wa zamani wa Msumbiji Joaqim Chissano na mwenzake wa Ghana John Kuffuor walizuru Malawi siku ya jumaatano kujaribu kuzima mvutano uliopo.

No comments: