Rais wa Marekani Barack Obama anazuru bara la Ulaya kwa mara ya kwanza tangu alipoingia madarakani. Matarajio ni makubwa miongoni mwa raia wa Ulaya na hata wanasiasa wanajitahidi kuwa na kipaji kama cha rais Obama. Lakini watalaam wanaonya dhidi ya kuwa na matarajio mengi mno katika ziara hiyo ya rais Obama.
Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Jamhuri ya Cheki na Uturuki zitamualika rais Obama wakati wa ziara yake barani Ulaya inayoanza hii leo na kumalizika Aprili 7. Mkutano wa nchi za G20 mjini London, mkutano wa jumuiya ya kujihami ya NATO mjini Strasbourg na Kehl ni mikutano muhimu atakayohudhuria rais Obama katika ziara yake ya Ulaya ambayo mbali na ziara ya Canada, inaweza kuelezwa kuwa ya kwanza kubwa tangu alipoingia madarakani Januari 20 mwaka huu.
Rais Obama anapendwa na kuungwa mkono na idadi kubwa ya raia wa Ulaya. Kiongozi wa shirika la Marshall Funds la Ujerumani mjini Washington Marekani, Craig Kennedy, anasema bado hajawahi kuona ziara ya rais wa Marekani barani Ulaya ikisubiriwa kwa hamu kubwa namna hii. Kennedy hata hivyo anasema kutakuwa na maswala nyeti katika ziara ya Obama.
"La kwanza bila shaka ni kuhusu mkakati wake wa kiuchumi, mipango ya uchumi ya utawala wake mpya. Na nadhani kwa jumla kuna wasiwasi kwamba fedha nyingi zinatolewa kuufufua uchumi lakini kuna sheria chache za usimamizi. Kiwango kikubwa cha fedha za kuufufua uchumi na madeni yatakayotokea, ni mambo yanayosababisha wasiwasi mkubwa."
Imeripotiwa kuwa utawala wa rais Obama utazitaka nchi za Ulaya ziwekeze zaidi, lakini ikulu ya Marekani imekanusha madai hayo. Mzozo kuhusu kiwango cha fedha zinazotolewa na kila nchi kuufufua uchumi haupo.
Michael Froman, mshauri wa rais Obama katika maswala ya kiuchumi anasema,"Hakuna mtu yeyote aliyeitaka, wala anayeitaka, nchi yoyote ile kuja mjini London kuahidi kufanya mengi zaidi hivi sasa. "
Swala ambalo huenda likazusha mvutano ni mkakati mpya wa serikali ya Marekani kuhusu Afghanistan. Viongozi wa Ulaya watakubaliana na mabadiliko msingi ya utawala wa Obama, lakini pia wanafahamu mengi yanatarajiwa kutoka kwao. Katika swala hili, ikulu ya Marekani imesisitiza kwamba haitasema hasa inachotaka.
Klaus Scharioth, balozi wa Ujerumani mjini Washington, anasema hakujatolewa ombi maalum kuhusu kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Afghanistan, lakini kila nchi mwanachama wa jumuiya ya NATO inatafakari mchango gani inayoweza kutoa nchini Afghanistan.
"Nadhani ni muhimu kuweza kuthibitisha kwenye mazungumzo hayo kwamba serikali mpya ya Marekani inathamini zaidi kuwashirikisha wananchi wake. Jambo ambalo naweza kulieleza kuwa ni utawala bora."
Sera kuhusu hali ya hewa zinaweza kuleta malumbano kati ya Marekani na Ulaya. Ikizingatiwa hali ya uchumi wa Marekani, watu wanajiuliza ikiwa swala la hali ya hewa litapewa kipaumbele katika utawala wa rais Obama. Ziara ya Obama barani Ulaya inaashiria mambo mengi. Dennis McDonough, mshauri wa rais Obama wa mawasiliano anasema kiongozi huyo wa Marekani anataka kuimarisha miungano yote na kujenga mingine mipya. Ziara ya Obama itakuwa ya kumuimarisha rais huyo, hadhi ya Marekani ulimwenguni na hususan kuwa tena na ushwawishi barani Ulaya.
Mbali na mazungumzo kuhusu mpango wa ulinzi dhidi ya makombora, ziara ya rais Obama mjini Prag huko Jamhuri ya Cheki ina maana nyeingine. Utawala wa rais George W Bush ulizishinikiza serikali za Poland na Jamhuri ya Cheki na kujaribu kutumia njia zote kuwashawishi raia wa nchi hizo waukubali mpango huo. Sasa hawana raha na inasaidia kwamba rais Obama atazuru Prag.
No comments:
Post a Comment