Mkutano muhimu wa kuamua hatma ya kampuni ya kutengeneza magari ya OPEL utaanza wakati wowote kuanzia sasa mjini Berlin, hapa Ujerumani. Makubaliano hayo yananinginia kwenye uzi mwembamba. Mapema leo, Kampuni ya Italia- FIAT ilijiondoa kwenye mazungumzo hayo, ikilalamikia ombi la ghafla la Ujerumani kuitisha fedha zaidi. Hata hivyo, FIAT imesema bado ina nia ya kuinunua OPEL na kwamba ombi lake la awali bado lipo mezani. Kampuni ya wawekezaji ya kutengeneza vipuri vya magari kutoka Canada na Austria, Magna, ambayo pia ilikuwa imetoa ombi la kuinunua OPEL, sasa inasemekana wanafikiria hata nao kujiondoa kwenye mazungumzo hayo. Waziri wa uchumi wa Ujerumani Karl Teodor tsu Guttenberg amesema muda unayoyoma, kwani tarehe ya Juni mosi iliyowekwa kwa kampuni mama ya General Motors kutangazwa muflis inakaribia.
Majadiliano haya yalikuwa tayari yameingia mvutano katika mkutano wa jana pale General Motors ilipotaka kwa ghafla ilipwe Euro milioni mia tatu za ziada. Ujerumani iliishtumu General Motors kwa ombi hilo, ikidai mazungumzo ya Opel hayapewi uzito na serikali ya Marekani.
No comments:
Post a Comment