Katika kile kinachoonekana Rais Jakaya Kikwete ameishiwa uvumilivu dhidi ya viongozi wasiotekeleza ipasavyo majukumu yao, amemtimua Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Enocy Mfuru, kwenye sherehe ya uzinduzi wa hoteli ya kitalii kwenye hifadhi ya Serengeti.
Badala yake amemtaka kwenda kushughulikia matatizo yanayoukabili mkoa wake, ikiwemo mapigano katika wilaya za Rorya na Tarime, madai ya mgodi wa madini wa North Mara na uchafuzi wa mazingira.
Tukio hilo lilitokea juzi wakati Rais Kikwete alipokuwa akifungua rasmi hoteli ya kisasa ya Bilila Kempinski iliyoko kwenye Hifadhi ya Serengeti.
Rais Kikwete alionyesha kushangazwa na kuwepo kwa mkuu huyo wa mkoa wa Mara kwenye sherehe hiyo pamoja na kwamba hifadhi ya Serengeti ipo mkoani mwake.
Kukatishwa kwa mkuu huyo wa mkoa kushiriki hafla hiyo ambayo Rais alikuwa mgeni rasmi, kulitangazwa na Rais mwenyewe wakati wa utambulisho wa wageni na kueleza kuwa hakuwepo hapo kwa kazi maalum.
Alimtaka mkuu huyo wa mkoa kwenda kutayarisha taarifa rasmi ya matatizo yanayoukabili mkoa wake na kisha amkabidhi kabla ya kuondoka.
Uchunguzi wa Nipashe kupitia vyanzo mbalimbali vya habari ulibaini kuwa mara baada ya agizo hilo la Rais Kikwete, mkuu huyo wa mkoa alilazimika kukutana na uongozi wa mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya Barrick ili kuona namna ya kuweka mambo sawa.
Mgodi wa North Mara umekuwa ukikabiliwa na matatizo na tuhuma mbalimbali kama vile askari wake kuwashambulia wananchi kwa risasi wanapokwenda eneo hilo, pamoja na kudaiwa kutiririsha sumu kwenye vyanzo vya maji yanayotumiwa na wananchi, hali ambayo inadaiwa kusababisha vifo vya watu kadhaa na mifugo.
Habari zinasema kuwa baada ya kikao hicho na uongozi wa mgodi wa North Mara, mkuu huyo wa mkoa alikutana na uongozi wa vijiji vya kata za Kemambo na Matongo kwa ajili ya kutaka kupata maoni yao. Hata hivyo inadaiwa viongozi hao walimwambia matatizo ambayo wamekuwa wakiyasema mara kwa mara kwa kila kiongozi wanayekutana naye lakini bila mafanikio.
Walimtaka kuhakikisha kuwa masuala ya mahusiano kati ya wananchi na mgodi yanaimarishwa hasa kwa kuwatengea
wachimbaji wadogo maeneo haraka kwa kuwa wamekuwa wakiahidiwa bila utekelezaji.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, wananchi hao walimtaka Kanali Mfuru asimamie ipasavyo malalamiko yao na si kukaa kimya huku wananchi wakizidi kufa, kupata ulemavu na mali za kampuni kuharibiwa.
Pia walimtaka ahakikishe kuwa suala la fidia kwa watu wanaoishi jirani na mgodi huo zinalipwa haraka ili kuwapunguzia madhara wayapatayo.
Uchunguzi uliofanywa na blog hili umebaini kuwa moja ya mambo ambayo yakifanyika yanaweza kupunguza vurugu, vifo na majeruhi wengi ni mgodi kuondoa mawe ya mchanga ambayo yanadaiwa ni uchafu, lakini wananchi wakienda kuyachukua ndipo mashambulizi huanza.
Baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na mgodi wamelieleza gazeti hili kuwa mbali na hilo pia ili kudumisha uhusiano mwema mgodi huo na serikali zinatakiwa kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo kwa kuwatengea maeneo yao sambamba na kupewa vifaa vya kisasa vya kuchimbia madini.
Aidha, suala la fidia pia linatakiwa kutazamwa kwa mapana hasa kwa watu wanaoishi karibu na mgodi huo ili waweze kuondolewa kupisha maeneo hayo kwa kuwa madhara wanayopata ni makubwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, ili kupunguza
misuguano isiyoisha kampuni hiyo imekubali kuyafanyia kazi baadhi ya mambo, hali ambayo huenda ikarejesha amani pamoja na utulivu katika eneo hilo.
Mkuu huyo wa mkoa wa Mara alipoulizwa na blog hii, ameweka mikakati gani kuhusiana na migogoro hiyo aling’aka na kusema, "Mimi nitakupaje taarifa wewe kama ndiye uliyenituma,hata aliyenituma sijampa wewe vipi,” alisema na kukata simu.
Hata hivyo ilibainika kuwa katika mkutano huo ambao ni wa kwanza kwake kukutana na viongozi wa eneo hilo licha ya kuwepo matatizo makubwa yakiwemo ya tindikali inayodhuru wananchi, haukuhudhuriwa na viongozi wengi kwa kuwa ulikuwa wa ghafla.
Aliahidi kukutana nao tena huku akisisitiza kuwa atahamia eneo hilo ili kuhakikisha amani inarejea sanjari na kujenga mahusiano mema, hata hivyo kitendo cha
kuanzia mgodini kisha kwa jamii bado kilionekana kuwakera baadhi ya viongozi kwa kuwa angepokea mambo ya jamii ndipo awaulize kama hayo wanayafahamu ama kuyafanya.
Mbunge wa jimbo hilo, Charles Mwera, akiongea kwa simu kutoka Mwanza akiwa safarini kuelekea jimboni kwake, alisema kuwa matumizi ya nguvu kupita kiasi yanasababisha eneo hilo kutopata amani ambayo wanaisaka kila kukicha.
Alisema kama watu wanakufa kwa tindikali na suluhu haijapatikana na mauaji mengine yanazidi kwa risasi ni lazima eneo hilo halitakuwa na amani na kuitaka serikali ifanye
uchunguzi wa kina si kusikiliza polisi wanavyotoa taarifa.
Hivi karibuni watu watatu wamekufa baada ya kupigwa risasi na askari polisi huku wengine zaidi ya saba wakijeruhiwa katika eneo la Nyabirama ,ambapo inadaiwa kuwa wengine walipigiwa majumbani kwao.
Mazishi yao yalifanyika juzi na kuhudhuriwa na watu wengi huku wakionyesha hali ya kutoridhishwa na mwenendo huo.
Rais Kikwete alitarajiwa kupewa taarifa hiyo ya mkuu wa mkoa kabla ya kuondoka kurudi Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment