July 13, 2009

OBAMA AMFAGILIA JK

Rais wa Marekani Barack Obama

Rais Barack Obama wa Marekani amemsifia Rais Dk.Jakaya Kikwete wa Tanzania, akimwelezea kama kiongozi wa mfano ambaye amefanya kazi nzuri ya kupeleka huduma za waziwazi kwa wananchi wake.

Rais Obama amesema kuwa Rais Kikwete ni mmoja wa viongozi wa Afrika walioonyesha uongozi thabiti ambao uko tayari kusonga mbele katika kuwaletea maendeleo wananchi wao.

Rais Obama ametoa sifa hizo kwa Rais Kikwete katika mahojiano na taasisi ya mawasiliano kwa njia ya inteneti ya AllAfrica.Com wakati akijiandaa kufanya ziara yake ya kwanza katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara, kwa kutembelea Ghana.

Rais Obama aliwasili Ghana usiku wa kuamkia jana (Ijumaa, Julai 10, 2009) kuanza ziara ya siku mbili ya kwanza katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Rais Obama anatarajiwa kuondoka Ghana leo kurejea kwao Marekani.

Kabla ya kutembelea Ghana, Rais Obama tayari alikwishakutembelea Bara la Afrika kwa kuzuru nchi ya Misri, iliyoko Afrika Kaskazini katika wiki za karibuni.

Rais Obama ambaye aliwasili Ghana akitokea katika Mkutano wa Nchi zenye Viwanda Vingi Zaidi Duniani wa G8 nchini Italia, aliiambia taasisi ya AllAfrica.Com katika mahojiano yaliyofanyika Ikulu ya Marekani kabla ya kuondoka kuelekea Russia, Italia na Ghana:

“Lazima kukumbuka kuwa pamoja na kwamba nitaitembelea Ghana kwa ziara hii, tayari nimemkaribisha Tsvangirai wa Zimbabwe katika Ofisi ya Rais wa Marekani. Tulikuwa na Rais Kikwete wa Tanzania kabla ya hapo katika Ofisi hii hii, na katika kila mkutano najaribu kuelezea ujumbe huo huo.”

Aliongeza Rais Obama: “Tumeona kazi nzuri sana inayofanywa na uongozi katika Tanzania ukielekeza nguvu zake katika kutoa huduma za wazi wazi na dhahiri kwa wananchi wake, na kila mahali ambako watu wanataka kujisaidia, na sisi tunataka kuwapo kama washirika wa uongozi.”

Rais Obama alimwalika Rais Kikwete kuwa kiongozi wa kwanza kabisa wa Bara la Afrika kukutana naye katika Ofisi ya Rais wa Marekani tokea kuapishwa kuwa kiongozi wa Marekani Januari 20, mwaka huu.

1 comment:

Anonymous said...

Malumbo hapo umechemsha bwana..kwani Obama alimtaja Kikwete kwenye hotuba yake ya Ghana???sasa kwa nini umeweka hiyo picha?..Usipotoshe Ukweli bwana!!

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22