Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na washirika wake kutoka jimbo la Bavaria wameshindwa kuondoa tofauti zao kuhusiana na suala la mkataba wa kuufanyia mabadiliko Umoja wa Ulaya, mkataba uitwayo wa Lisbon.Katika mkutano wao uliyofanyika jana, chama cha Christian Social Union cha Jimbo la Bavaria, CSU, ambacho ni chama ndugu na kile cha Kansela Merkel cha Christian Democratic, CDU, vilishindwa kuondoa tofauti zao kuhusiana na suala hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa tarehe 27 Septemba.
Chama hicho cha CSU kina wasi wasi na mabadiliko hayo, kikisema kuwa yatatoa mamlaka zaidi kwa umoja huo dhidi ya nchi wanachama.
Lakini chama cha Kansela Merkel cha CDU na kile cha Social Demokrat vinavyounda serikali ya mseto, vinaunga mkono mkataba huo ambapo vingependa kuona unaridhiwa kabla ya uchaguzi huo mkuu wa Ujerumani.
Hatua hiyo itamfedhehesha Kansela Merkel na huenda ikazipa nguvu nchi zenye wasi wasi na mkataba huo, kama vile Jamuhuri ya Czech na Poland ambazo hazijauridhia, zikitaka kwanza nchi zote wanachama ziukubali.
Ni nchi nne tu wanachama wa umoja huo ambazo mpaka sasa hazijahuridhia, ikiwemo Ireland ambayo wananchi wake waliukataa katika kura ya maoni mwaka uliyopita na inatarajiwa kupiga tena kura hapo Oktoba mbili mwaka huu.
Lakini Kansela Merkel alikuwa na matumaini ya Ujerumani kuuridhia mkataba huo, mara baada ya hukumu ya mahakama ya katiba mapema mwezi huu ambapo ilitupilia mbali madai ya wale wanaoupinga ya kwamba unakiuka katiba ya nchi. Hata hivyo, ilielekeza kufanyika kwa marekebisho katika baadhi ya sheria kabla ya kupitishwa rasmi na bunge.
Akizungumza mara baada ya kushindwa kuafikana na washirika wake jana usiku huko Bavaria, Kansela Merkel amesema walijadiliana na mwenyekiti wa chama cha CSU wanachoshirikiana katika kuunda serikali, Horst Seenhofer.
Amesema walijadiliana kuhusiana na hukumu hiyo ya mahakama ya katiba, na kuongeza kuwa vyama hivyo vimekubaliana kuwa na msimamo utakaoisaidia serikali yao kulinda maslahi ya bunge.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa CSU, Horst Seenhofer, alisema watakakia kuwa imara na kuendelea na majadiliano endelevu kuhusiana na suala hilo.
Ama kuhusiana na mvutano uliyojitokeza kati ya chama chake cha Christian Demokrat na chama ndugu cha Christian Social, Kansela Merkel alisema.
Naamini kwamba hapa kila mtu anafahamu kuwa CDU na CSU ni lazima watafikia muafaka. Mimi, kama kiongozi wa serikali, nimeweka wazi wapi yalipo maslahi ya serikali. Wabunge nao wameweka wazi kile ambacho walikuwa na wasi wasi nacho, na, kwa hivyo, sioni kuwepo ugumu wowote katika suala hili´´.
Aidha Kansela Merkel amesema wamekubaliana kuwepo kipindi cha muda maalum kujadiliana ambacho amesema ni nafasi nzuri ya kufikia muafaka kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment