Majadiliano juu ya hatima ya kampuni ya magari Opel iliyokumbwa na matatizo ya kifedha, yamemalizika bila ya mafanikio.Sasa kuna hofu kuwa hatima ya kampuni hiyo huenda isijulikane mpaka baada ya uchaguzi wa Ujerumani.
Hata hivyo Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Karl-Theodor zu Guttenberg anaamini kuwa bado upo uwezekano kwa kampuni ya Opel kujitenga na kampuni mama General Motors. Katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Ujerumani ZDF jana usiku alisema ujumbe uliopokewa kutoka wakuu wa kampuni hiyo ni kwamba General Motors inaendelea kutafuta mwekezaji. Waziri zu Guttenberg akaongezea:
"Kwa upande wetu,serikali imetekeleza jukumu lake na limefanikiwa pia kuboresha masharti, hasa kuhusu mtaji wa wawekezaji - lakini serikali ya Ujerumani haiwezi kuiamulia General Motors."
Majuma ya hivi karibuni General Motors iliyopangwa upya baada ya asilimia 60 ya hisa zake kumilikiwa na serikali ya Marekani, imekuwa ikishauriana na serikali ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kujaribu kuafikiana kuhusu wawekezaji wawili wanaogombea kuinunua Opel: kampuni ya Kanada, Magna inayotengeneza vipuri vya magari ikiungwa mkono na benki ya Kirusi Sberbank na wa pili ni kampuni ya uwekezaji RHJ International yenye makao yake mjini Brussels Ubeligiji.
Lakini General Motors iliyoepuka chupuchupu kwenda muflisi mapema mwezi wa Julai, sasa inaamini kuwa ina nafasi nzuri ya kuendelea kuwa na usemi katika sekta ya magari kote duniani na haitaki kuipoteza nafasi hiyo. Akibanwa na kizungu mkuti hicho, mjumbe wa General Motors John Smith hiyo jana, alikutana na maafisa wa Ujerumani.
Lakini General Motors au kwa ufupi GM kwanza itapaswa kutafuta fedha za kutosha ili viwanda vya Opel viweze kuendelea kufanya kazi na wataalamu wa kiuchumi wanakumbusha kuwa tangu mwaka 2005,GM imepata hasara ya dola bilioni 90 na mikopo hutolewa kwa makampuni yaliyo imara kifedha.
Kufuatia mkutano wa jana usiku mjini Berlin, serikali ya Ujerumani iliyokuwa ikiiunga mkono Magna,sasa inasemekana kuwa ipo tayari kuizingatia kampuni ya RHJ International. Kampuni hiyo lakini itapaswa kushirikiana na mwekezaji muhimu katika sekta ya viwanda vya magari. Barani Ulaya,kama asilimia 50 ya wafanyakazi 50,000 wa Opel wapo Ujerumani. Hali ya kutatanisha kuhusika na hatima ya Opel imesadif katika wakati ambapo vyama vikuu vya kisiasa nchini Ujerumani vinakabiliwa na mtihani wa uchaguzi wa majimbo mwishoni mwa juma hili na uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi wa Septemba
No comments:
Post a Comment