Timu ya Togo haiondoki Angola, licha ya kuuwawa kwa watu watatu wa ujumbe wao, katika shambulizi Cabinda.
Timu ya taifa ya soka ya Togo imeamua itasalia Angola na kushiriki katika dimba la kombe la Mataifa ya Afrika, linaloanza leo, nchini Angola. Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo Thomas Dossevi aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa wachezaji wa timu hiyo walijadiliana na kufikia uamuzi huo, licha ya mwito wa serikali yao kuwataka waondoke Angola, baada ya basi lao kushambuliwa na watu waliokuwa na silaha. Dossevi alisema watashiriki kama heshima kwa wenzao waliouawa katika shambulizi hilo la Ijumaa.
Watu watatu waliuawa, ikiwemo Kaimu mkufunzi wa timu hiyo na dereva wao kufuatia basi lao kuvamiwa na waasi wa kundi la FLEC linalopigania uhuru wa kujitenga katika eneo hilo la Cabinda. Watu wengine tisa walijeruhiwa ikiwemo golikipa wa timu hiyo ya Togo na beki wao mmoja. Togo watacheza mechi yao ya kwanza kesho huko Cabinda dhidi ya Ghana. Dimba hilo la Afrika linalojumuisha mataifa 16, linaanza leo, na mechi ya kwanza itakuwa kati ya wenyeji Angola na Mali huko Luanda.
1 comment:
oya hiyo video haioneshi
Post a Comment