November 23, 2010

Wiki ya kilio na kicheko

Baada ya kumteua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kumwapisha Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, Rais Jakaya Kikwete anatarajia wakati wowote kati ya leo na kesho kuteua baraza lake la mawaziri.

Wakati wa kulizindua Bunge la 10 Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema kuwa anatarajia kuunda Baraza la Mawaziri hivi karibuni na kudokeza sifa wanazotakiwa kuwa nazo atakaowateua kuwa mawaziri.

Bila shaka Rais Kikwete atakuwa amezitumia siku za mwisho wa wiki kushauriana na wasaidizi wake wakuu Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Pinda, kuhusu uundaji wa Baraza la Mawaziri.

Rais Kikwete aliliambia Bunge kuwa katika kuunda Baraza la Mawaziri, dhamira yake ni kupata serikali makini.

“Katika siku chache zijazo nitaunda baraza la mawaziri.

Dhamira yangu ni kwamba tupate Serikali makini, yenye watu waadilifu na wachapakazi hodari. Watu ambao wataongoza nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mipango ya Serikali kwa umahiri mkubwa.

“Watu ambao wataondoa urasimu katika Serikali, watakuwa karibu na watu na watashirikiana vizuri na Waheshimiwa Wabunge bila kujali vyama vya siasa wanavyotoka, “ alisema Rais.

Tangu Ijumaa wananchi wamekuwa wakisubiri kwa hamu kuona sura za mawaziri watakaoteuliwa baada ya Rais Kikwete kudokeza sifa za baraza atakaloliunda.

Baadhi ya majina ya wabunge wa CCM yamekuwa wakitajwatajwa kuhusiana na uteuzi huo.

Hata hivyo, pamoja na Rais Kikwete kutaja sifa za watakaoteuliwa, uzoefu wa muda mrefu tangu wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza hadi ya nne unaonyesha kuwa kigezo kikubwa ambacho kinatumika katika uteuzi wa baraza hilo ni umoja wa kitaifa.

Kwa kuzingatia hilo, kila mkoa umekuwa unapewa nafasi angalau moja kwa lengo la kuhakikisha kwamba Serikali inaundwa na wawakilishi kutoka mikoa yote nchini.

Vipaumbele alivyovitaja Rais Kikwete kuwa ndio mwelekeo wa serikali yake kwa miaka mitano ijayo ni:

1. Kudumisha umoja, amani, usalama na kudumisha Muungano.

2. Kuendeleza juhudi za kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini kwa kuchukua hatua thabiti za kuharakisha mapinduzi ya kilimo, uvuvi, ufugaji na viwanda.

3. Kuendelea kuongeza jitihada za kuwawezesha kiuchumi wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki na kunufaika na uchumi unaokua na kubore sha mipango iliyopo ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wote wanaotaka kujiajiri.

4. Kikwete alisema serikali itaendelea kujenga na kuimarisha sekta binafsi nchini na kutengeneza mazingira mazuri zaidi ya ushirikiano na sekta ya umma.

5. Tanzania kutumia nafasi yake ya kijiografia kunufaika na matumizi ya miundombinu ya nchi kwa kupitisha bidhaa na

huduma za nchi majirani.

6. Kuendeleza juhudi kuhakikisha kwamba taifa linanufaika na rasilimali za juu na chini.

7. Kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa pamoja na kuimarisha nidhamu ya matu mizi ya fedha na mali za umma.

8. Kuendeleza juhudi za kupanua ursa za elimu kwa vijana kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu hasa masomo ya sayansi kwa ngazi zote.

9. Kuimarisha huduma za jamii kama afya, maji, barabara, na umeme.

10. Kuimarisha utawala bora, sheria na haki za bindamu na kupiga vita ubadhirifu.

11. Kukuza ushirikiano na mataifa mengine ya nje;

12. Kukuza mara dufu juhudi za kuhifadhi mazingira;

13. Kulinda na kukuza mafanikio yaliypofikiwa na serikali ya awamu ya nne na mafanikio yote tangu uhuru.

Kutangazwa kwa Baraza la Mawaziri kutawafurahisha watakaoteuliwa na kuzua kilio kwa waliotarajia kuteuliwa, lakini matarajio yao kugonga mwamba.

Kilio kitakwenda kwa waliokuwa mawaziri katika baraza lililomaliza muda wake. Akizungumza na NIPASHE jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema shughuli ya kutangaza Baraza la mawaziri ni ya Rais na kwamba atatangaza atakapoamua.

No comments: