MANENO MACHAFU NA KASHFA HAZINA NAFASI KATIKA KIWANJA HIKI. TUNAKARIBISHA MAONI YENYE KUJENGA NA KUELIMISHA JAMII.
February 01, 2013
Uhuru Marathon: Inakumbusha tulipotoka, tulipo, tunapokwenda
Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani, kila mara wanakutana katika vikao vya kimataifa kusaka amani, bila amani hakuna kitu chochote kinachoweza kufanya nchi isonge mbele.
Utasongaje mbele wakati kila saa ni migogoro na vita? Lakini Watanzania tumejaliwa kwa kiasi kikubwa kuwa na amani, ambayo kwa sasa kuna baadhi ya watu wanataka kuichezea. Ni kama vile wamechoka nayo.
Lakini wakati kukiwa na migogoro mingine ambayo haina tija, kuna kitu ambacho kimeanzishwa ili kuwakumbusha Watanzania kuhusu misingi halisi tuliyowekewa na waasisi wa Taifa hili.
Hiki si kingine isipokuwa ni mbio za Uhuru Marathon, ambazo zitafanyika mwishoni mwa mwaka huu huku Rais Jakaya Kikwete kwa kuona umuhimu wake naye ameamua kushiriki kama kinara na jemedari wa Taifa hili ambapo mara kwa mara amekuwa akiwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kuenzi amani iliyopo..
Akithibitisha hilo, Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck, anasema lengo la mbio hizo ni kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kukumbuka, kuzingatia na kuuenzi urithi waliaochiwa na viongozi waliopigania uhuru wa nchi.
Anasema urithi huo ambao utakuwa ukikumbukwa kila mwaka kupitia mbio hizo, ni upendo, mshikamano, umoja na amani iliyopo. Melleck anasema mbio hizo zitakuwa zikifanyika kila mwaka na zitaanza rasmi siku ya tarehe 08/12/2013 na zitatanguliwa na shamrashamra za kanda zote za Nchi yetu.
Hilo lilithibitishwa pia na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara , ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati zinazinduliwa jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi wa mbio hizo ulienda sambamba na kuzinduliwa rasmi kwa mtandao wa Uhuru Marathon ambao utakuwa na habari za kila aina kuhusu mbio hizo na washirika wake.
Dk. Mukangara alipongeza wazo la kuanzishwa mbio hizo ambazo zitakuwa zikifanyika kila mwaka, lengo likiwa ni kudumisha umoja, amani na upendo miongoni mwa Watanzania na kuuenzi uhuru wetu.
Waziri alikiri, kwa sasa kuna mbio nyingi za marathon hapa nchini, lakini hakuna ambaye alikuja na wazo zuri la kuanzisha mbio kama hizo za kuuenzi uhuru wetu na kudumisha amani nchini.
“Nawapongeza waandaaji wa mbio hizi ambao ni vijana wa Kitanzania waliokuja na wazo hili zuri la kuanzisha mbio za uhuru. Tunazo mbio nyingi sana hapa nyumbani, lakini hatukuwa tumewaza kuanzisha mbio zinazolenga kuuenzi uhuru wetu na kudumisha amani yetu.
“… Kwa niaba ya Serikali, napenda kusema wazi kuwa tumefurahishwa sana na wazo hili la kuanzisha mbio hizi za Uhuru na nichukue fursa hii kuwaomba wadau na wapenda maendeleo ya michezo kuungana na taasisi hii kufanikisha mpango huu ili uweze kuwa na mafanikio.
“Serikali bado itaendelea kuweka miongozo na mazingira rafiki ya kushirikiana na wadau wenye nia nzuri ya kuendeleza michezo nchini. Nina hakika waheshimiwa mawaziri, wabunge, viongozi mbalimbali wa Serikali, mashirika binafsi na viongozi wa dini wote watajitokeza kushiriki mbio hizi,” alisema.
Hapa ndipo tunapoweza kusema kwamba, fikiria mbio zozote kubwa duniani kama vile London Marathon nchini Uingereza, Paris Marathon, Ufaransa au zile zingine zenye kupendwa na wengi zaidi duniani za Berlin Marathon zinazofanyika Ujerumani kila mwaka, lakini Uhuru Marathon ni zaidi ya mbio.
Kwani mashindano yote haya ni ya kutukuka, kutokana na kushirikisha wanariadha wenye majina makubwa duniani, huku kukiwa na ushindani mkubwa zaidi miongoni mwa washiriki.
Lakini kwa sasa Tanzania ina cha kujivunia zaidi kwa ujio wa mashindano ya mbio Uhuru Marathon.
Upekee wa shindano hilo la Uhuru Marathon ni kutokana na aina ya washiriki wake, pamoja na kupewa tafu kubwa na waandaaji wa mashindano ya Berlin Marathon, ambao wanataka kuiona Tanzania inatangazwa zaidi.
Hivyo, shindano la Uhuru Marathon, lina nafasi kubwa ya kuwabeba Watanzania kwa kutangazika zaidi, hasa ukichukulia uzoefu mkubwa walionao waandaaji wa Berlin Marathon ikiwa pamoja na kuchangia kudumisha amani na upendo nchini.
Mratibu wa mbio hizo, Innocent melleck anasema, ana imani mbio hizo zitajizolea umaarufu mkubwa, kutokana na jinsi zitakavyoteka hisia za watu mbalimbali, wakiwemo wanamichezo.
Katika mbio hizo, zitakazowashirikisha watu wa kada mbalimbali, zitakuwepo pia mbio za kilomita 3, kilomita 5, Half Marathon kilomita 21 pamoja na Full Marathon yenyewe kilomita 42.
Mratibu huyo anasema mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji ya aina mbalimbali.
“Hapa tunachotaka kufanya katika mbio za kilomita 3 ni kuwaomba kama vile viongozi maarufu wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wetu ili kushiriki, kwa kudumisha amani na upendo.
“Pia tutahakikisha kama mbio za kilomita 5, zinakuwa kwa ajili ya kuchangia watu wenye mahitaji mbalimbali na tayari tuna uhakika mkubwa wa wanariadha maarufu zaidi duniani kushiriki,” anasema.
Mratibu huyo anafafanua kuwa wamejipanga mno katika hilo ili kuhakikisha wanafanya mambo makubwa zaidi na ambayo yataleta tija kwa taifa.
Wakati Uhuru Marathon ikitambulishwa bungeni, kiongozi aliyeonekana kufurahishwa zaidi na hilo ni Spika Anne Makinda, ambaye hakuishia kulimwagia sifa tu, bali alitaka hata viongozi wahakikishe wanalifanikisha.
Ni wazo zuri hasa katika kipindi hiki ambacho tunapigania amani na mshikamano miongoni mwetu, tunatakiwa kuenzi mashindano kama haya ili kutufanya tuwe wamoja zaidi,” alisema Spika Makinda.
Msaada wa Berlin Marathon
Melleck anasema, wamefanya mazungumzo na waandaaji wa mashindano ya Berlin Marathon, kwani hilo ni moja kati ya mashindano makubwa zaidi duniani, likiwa linashirikisha washiriki mbalimbali walio maarufu zaidi.
Shindano la Berlin Marathon au maarufu zaidi kwa jina la BMW Berlin Marathon kutokana na kudhaminiwa na kampuni ya BMW ni maarufu zaidi ndani ya Ujerumani na duniani kwa ujumla.
Shindano hilo la Full Marathon la kilomita 42.195 ambalo linawashirikisha wanariadha wa kulipwa na wale wa ridhaa, lilianza kwa mara ya kwanza mwaka 1974 na linafanyika kila wiki ya mwisho wa Septemba kila mwaka.
Shindano hili kwa umaarufu wake, mwaka 2008 lilishirikisha wanariadha takriban 40,827 kutoka mataifa 107, huku waliomaliza mbio wakiwa 35,913 na lina zawadi mbalimbali za kuvutia.
Uhuru Marathon je?
Melleck anasema, ushirikiano wa Berlin Marathon una maana kubwa, kwani itasaidia kuitangaza zaidi Tanzania na kuifanya dunia itambue umuhimu wa amani, upendo, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
“Wanariadha wengi watashiriki katika mbio hizi, wengi wakiwa maarufu zaidi duniani, pamoja na viongozi wa kada mbalimbali na hivyo kutimiza lengo tulilojiwekea.”
Mratibu huyo anasema, kuna kila haja kwa Watanzania, kuyathamini mashindano hayo, kwani yana lengo la kuwafanya wawe wamoja zaidi, hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho kuna majaribu ya kila aina.
“Waasisi wetu wa taifa na wale waliopigania uhuru, walikuwa na malengo mengi na tunatakiwa kuyadumisha hayo, hilo ndilo Uhuru Marathon inalotakapigania,” anasema.
Kwa Watanzania itakuwa faraja zaidi, hasa ukichukulia jinsi taifa linavyoweza kufaidika kwa kuzalisha pia wanariadha wa aina mbalimbali.
Hivyo Uhuru Marathon ni zaidi ya mbio, kwani inatukumbusha tulipotoka, tulipo na tunapokwenda!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22
-
NDUGU,JAMAA, MARAFIKI NA WADAU WA BLOG HII YA JAMII NASIKITIKA KUWATAARIFU YA KUWA NIMEPATWA NA MSIBA WA MAMA YETU MPENDWA BI KHADIJA( NA...
-
blog hii bado inatengenezwa na unakaribishwa kwa maoni. Pia unakaribishwa kuangalia website yetu mpya http://kilimanjarostars.de/ .
No comments:
Post a Comment