April 19, 2008

Bwana Vijisenti

Mh. Chenge akitafakari kuhusu Vijisenti vya Umma

Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, amegeuka bubu, hataki kuzungumza na waandishi, sasa anawakimbia. Bw. Chenge maarufu kwa jina la `bilionea wa vijisenti`, alifanya kioja hicho jana jijini Dar es Salaam baada ya kufunga Mkutano wa Kimataifa wa masuala ya Usalama wa Vyombo vya Usafiri Baharini (IMO). Mkutano huo ulioshirikisha mashirika mbalimbali ya kupambana na uhalifu wa aina mbalimbali duniani, wadau walitiliana saini Mkataba wa Makubaliano ya Usalama wa Vyombo vya Usafiri Magharibi mwa Bahari ya Hindi. Bw. Chenge ambaye alionekana mpole mno muda wote wa hotuba yake, alipomaliza alitoka nje tofauti na kawaida yake kuzungumza na waandishi nje ya ukumbi, jana aliwaona waandishi hao kama adui zake. Waandishi wakiwa nje ya ukumbi huo jijini Dar es Salaam, walimzonga Waziri Chenge huku wengine wakimuwekea vipaza sauti, lakini aliamsha mdomo wake mara moja tu na kusema ``sizungumzi chochote`` huku akishuka kwa kasi ngazi za ghorofa ya kwanza ulipo ukumbi huo, akisindikizwa na wasaidizi wake. Hata hivyo, waandishi wa habari huku wakiendelea kuwa na matumaini kwamba huenda Waziri huyo atajibu maswali yao akiwa nje, hali ilikuwa tofauti, kwani alifunguliwa mlango wa gari lake na kuingia haraka haraka na kuondoka. Aprili 12, mwaka huu, gazeti la The Guardian la Uingereza, liliandika habari kuwa, Waziri Chenge amejilimbikizia dola zaidi ya milioni moja (zaidi ya Shilingi bilioni moja) kwenye benki moja iliyopo kisiwa cha Jersey, Uingereza. Gazeti hilo lilieleza kuwa, inasadikiwa fedha hizo ni sehemu ya mgawo wa rushwa iliyotokana na ununuzi wa rada ya serikali ya Tanzania, wakati huo Bw. Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Wakati huo huo, Mwenyekiti DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amemshauri Bw. Chenge, kujiuzulu. Aidha, Mchungaji Mtikila amesema ameanza kukusanya mikataba mibovu aliyodai ilisababisha hasara ya mabilioni ya fedha kwa serikali kwa nyakati tofauti. Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari. Alisema pamoja na kumshauri Bw. Chenge ajiuzulu, ni vyema akarudisha fedha anazotuhumiwa kumiliki ili kulinda heshima ya taifa. Akizungumzia mikataba inayokusanywa na kupitiwa kutoka kwenye taasisi na wizara, alisema ni pamoja na ile ya umeme ya Richmond, Dowans, IPTL, Songas, Aggreko na Net Group Solutions. Mingine alisema ni ya madini iliyosainiwa kati ya Benki Kuu (BoT) na Hazina ile ya Kampuni ya Simu Nchini (TTCL) pamoja na ya ununuzi wa rada na ndege ya Rais, vyakula feki vyote vikigharimu mabilioni ya fedha. Alisema mikataba hiyo itapitiwa kwa umakini na kamati maalumu pamoja na wanasheria alioafikiana nao ili kuiweka wazi kwa wananchi. Alisema wanasheria zaidi ya 40 wanahitajika kufanya kazi hiyo. ``Tunahitaji wanasheria wasiopungua 20 ili kukamilisha idadi ya 40 tunayohitaji ambao wako tayari kwa ukombozi,`` alisema.

1 comment:

Anonymous said...

Kaka mwenye blog umeoa?mie NAKUPENDA! mdau Berlin!

 Wale wajanja wote tunakutana Leverkusen 24.09.22