Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imetoa wito wa kuidhinisha mpango wa fedha utakaogharimu euro bilioni 200 kwa minajili ya kuuchagiza uchumi wa bara la Ulaya unaodorora.Pendekezo hilo linajikita zaidi katika punguzo la kodi pamoja na kuongeza bajeti za mataifa wanachama ili kuongeza ununuzi.
Euro bilioni 170 za kiwango hicho zitafadhiliwa na bajeti za kitaifa za nchi wanachama na bilioni 30 zilizosalia zitasimamiwa na bajeti za mabenki ya Umoja wa Ulaya na Benki ya Uwekezaji za Ulaya.
Kwa mujibu wa Rais wa Kamisheni ya Ulaya Jose Manuel Barroso sehemu kubwa ya hatua hizo huenda zikaanza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka ujao na zilizosalia katika mwaka wa 2009 hadi 2010.
Kamisheni ya Umoja wa Ulaya inataraji kuzishawishi nchi wanachama kuuidhinisha rasmi mpango huo katika kikao kinachopangwa kufanyika tarehe 11 na 12 mwezi Disemba.
Itakumbukwa kuwa Ujerumani imepinga vikali hatua hiyo.
No comments:
Post a Comment