March 14, 2009

PINDA NA MIKATABA FEKI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameshuhudia mkataba mbovu unaonukia ufisadi katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT), jijini Dar es Salaam. 

Ufisadi huo unafanywa kupitia mkataba uliofikiwa kati ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Mkandarasi, kampuni binafsi ya Smart Holdings, inayomilikiwa na familia ya Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Kingunge Ngombale-Mwiru. 

Mkandarasi huyo alipewa zabuni ya kukusanya mapato kituoni hapo na amekuwa akifanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka mitano sasa. 

Kwa mujibu wa Meneja wa UBT, Fadhili Izumbe, katika mkataba huo, mkandarasi huyo hulipa Sh. milioni 1.5 kwa Halmashauri ya Jiji hata kama atakusanya mapato ya Sh. bilioni 1 kituoni hapo kwa siku. 

Waziri Mkuu alishuhudia ufisadi huo alipotembelea kituo hicho jana, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo katika Jiji la Dar es Salaam, iliyoanza juzi. 

Pinda alishangazwa na kushtushwa na utendaji mbovu wa uongozi wa UBT, mkataba huo na namna mkandarasi huyo alivyopatikana. 

Alifikia hali hiyo, baada ya kupewa taarifa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Abubakari Kingobi, kuhusu hali ya utendaji wa uongozi wa UBT, ukusanyaji wa mapato, mkataba wa mkandarasi na maendeleo ya kituo hicho. 

``Kituo hiki ni kikubwa sana, kuna maswali mengi ninawauliza hamna majibu. Hizi hela mnazopata ni kwa manufaa yenu au wananchi? Mmempataje huyu mkandarasi? Mikataba ikoje? Naomba kujua,`` alisema Pinda. 

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Kingobi hakuweza kujibu lolote, badala yake akamwita Meneja wa UBT, Izumbe ambaye naye hakutoa majibu, badala yake aliishia kusema: ``Aah!`` 

Katika taarifa yake, Izumbe alisema kwa mujibu wa mkataba, mkandarasi huyo hutoa Sh. milioni 1.5 kwa Halmashauri ya Jiji kwa siku, taarifa iliyomshangaza Pinda na kumfanya ahoji: ``Hata kama anakusanya Sh. bilioni 1 anatoa Sh. milioni 1.5? Na kwa nini mkataba utamke shilingi badala ya asilimia?`` 

Kutokana na hali hiyo, Pinda aliiagiza Halmashauri ya Jiji na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuupitia upya mkataba huo ili kuondoa maswali yasiyokuwa na majibu. 

Kwa siku mabasi zaidi 400 husafirisha abiria kutoka UBT, teksi 100 na watu zaidi ya 2,000 huingia. Pia kuna maduka ya vinywaji (Baa na Grosari), maduka ya kawaida, hoteli, `vioski`, gereji, ambavyo vyote hulipa ada za viwango mbalimbali. 

Naye Katibu wa Kamati ya Ulinzi UBT, Kibakuli Ngonyani, alimweleza Pinda kuwa askari mgambo wamekuwa wakishirikiana na wezi na ndio maana wimbi la wizi limeongezeka kituoni hapo. Pinda aliagiza tatizo hilo lifanyiwe kazi mara moja. 

Akiwa katika soko la Tandale, Pinda aliiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuweka uongozi mpya ili mapato yanayokusanywa sokoni hapo yaongezeke. 

Pinda aligiza suala hilo baada ya kutoridhishwa na uongozi uliopo, ambao umekuwa ukikusanya Sh. milioni 1 kwa mwezi, huku soko likikabiliwa na ukosefu wa umeme, maji, vyoo na miundombinu mbingine. 

``Hela zinazokusanywa ni nyingi, lakini zinawanufaisha wachache,`` alisema Pinda. 

Kuhusu maji yanayojaa katika eneo la Msasani Bonde la Mpunga, Pinda alisema tatizo hilo liko ndani ya uwezo wa serikali na akaahidi kulifanyia kazi. 

Hata hivyo, aliiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, kwamba wanapotoa vibali wahakikishe wawekezaji wanafanya tathmini ya mazingira katika eneo hilo. 

Mkazi wa eneo hilo, Godfrey Bagenda, alimweleza Pinda kuwa wananchi wenye asili ya Kiasia wamekuwa wakiwanyanyasa na kusema kuwa kuna siku watadai haki zao kwa nguvu. 

Katika ziara ya jana, Waziri Mkuu alitembelea eneo la Kigogo, ambako wakazi wake walionyesha kukerwa na dampo lililoko katika eneo hilo. 

Kutokana na hali hiyo, Pinda aliagiza dampo hilo liwe limehama ifikapo Septemba, mwaka huu.

No comments: